Arteta aondolewa benchi Arsenal

Muktasari:
- Kocha huyo Mhispaniola huyo alionyeshwa kadi ya njano kwenye mechi dhidi ya Newcastle United baada ya kuupiga mpira. Kadi hiyo ya njano ilikuwa ya tatu Arteta kuonyeshwa msimu huu.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Arsenal, Mikel Arteta hatakuwapo kwenye benchi la ufundi la timu hiyo katika mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu England msimu huu kutokana na kutumikia adhabu ya kadi tatu za njano.
Kocha huyo Mhispaniola huyo alionyeshwa kadi ya njano kwenye mechi dhidi ya Newcastle United baada ya kuupiga mpira. Kadi hiyo ya njano ilikuwa ya tatu Arteta kuonyeshwa msimu huu.
Na kutokana na hiyo, Arteta sasa atatumikia adhabu ya kukosa mechi moja.
Hiyo ina maana hatakuwa kwenye benchi la ufundi wakati Arsenal itakapokipiga na Southampton katika mechi ya mwisho ya msimu ya Ligi Kuu England. Kocha msaidizi, Albert Stuivenberg atabeba majukumu ya kuiongoza Arsenal kwenye mechi hiyo ambayo bosi wake atakosa.
Hata hivyo, hilo halimsumbui sana Arteta kwa sababu timu yake tayari imeshajihakikishia kumaliza msimu kwenye nafasi ya pili na kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Bao pekee la kiungo ghali wa miamba hiyo ya Emirates, Declan Rice wakati Arsenal ilipoichapa Newcastle 1-0 na lilitosha kuipa Gunners tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Kwa maana hiyo, Arsenal hata kama itapoteza mchezo wa mwisho dhidi ya Southampton haitakuwa na athari yoyote kwao.
Arsenal sasa inataka kurudi kivingine msimu ujao baada ya huu kuumaliza mikono mitupu kwa mara nyingine bila ya taji lolote. Kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, Arsenal ilikomea kwenye hatua ya nusu fainali, ilipotolewa na Paris Saint-Germain, ambayo itacheza fainali na Inter Milan.