Lazima kieleweke usiku wa Ulaya

Muktasari:
- Real Madrid itakwenda ugenini kwenye mechi hiyo ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 2-1 ilioupata kwenye mechi iliyopita, lakini vijana wa Diego Simeone, Atletico wamekuwa wagumu kukubali kupotea kirahisi jambo linalofanya mechi hiyo kuwa na mtazamo wa “haijaisha hadi iishe kabisa”. Ni hatari.
MADRID, HISPANIA: KIVUMBI na jasho. Ndicho unachoweza kusema kuhusu kipute cha Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya mtoano kitakachopigwa usiku wa leo Jumatano, huku wengi wakisikilizia kitakachokwenda kutokea Wanda Metropolitano wakati Atletico Madrid itakapokipiga na Real Madrid kwenye Madrid Derby ya Ulaya.
Real Madrid itakwenda ugenini kwenye mechi hiyo ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 2-1 ilioupata kwenye mechi iliyopita, lakini vijana wa Diego Simeone, Atletico wamekuwa wagumu kukubali kupotea kirahisi jambo linalofanya mechi hiyo kuwa na mtazamo wa “haijaisha hadi iishe kabisa”. Ni hatari.
Shughuli nyingine pevu ya usiku wa leo, itakuwa huko Ufaransa, ambapo Lille itakuwa mwenyeji kuikaribisha Borussia Dortmund kutoka Ujerumani. Mechi ya kwanza iliyofanyika Ujerumani ilimalizika kwa matokeo ya sare ya 1-1, hivyo kipute hicho ni kama kinaanza upya kabisa.
Kwa Arsenal wao watakuwa na kazi nyepesi tu ya kukamilisha ratiba mbele ya PSV uwanjani Emirates baada ya kushinda 7-1 katika mchezo wao wa kwanza uliofanyika Uholanzi.
Aston Villa yenyewe pia itakuwa na kazi ya kulinda matokeo yao ya mchezo uliopita dhidi ya Club Brugge iliposhinda 3-1, wakati itakaporudiana na miamba hiyo uwanjani Villa Park, lakini macho na masikio ya wengi yataelekea huko kwenye Madrid derby ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.