Lamine Yamal amejifunza kutokana na makosa yeke
Muktasari:
- Kwa mara ya kwanza katika maisha yake ya soka, Yamal alijikuta akiwa kitovu cha hasira za uwanja mzima, baada ya kauli alizotoa kabla ya ushindi wa Real Madrid wa mabao 2–1 jana Jumapili Oktoba 26, 2025 kuwa sababu ya ukosoaji mkubwa katika mji mkuu wa Uhispania.
Maneno ya mshambuliaji wa Barcelona, Lamine Yamal kabla ya mechi ya El Clásico yalizua gumzo kubwa kuliko hata kiwango chake uwanjani, baada ya Barcelona kupoteza mechi hiyo na huenda kijana huyo mwenye umri wa miaka 18 anaweza kupata funzo muhimu kwa siku zijazo.
Kwa mara ya kwanza katika maisha yake ya soka, Yamal alijikuta akiwa kitovu cha hasira za uwanja mzima, baada ya kauli alizotoa kabla ya ushindi wa Real Madrid wa mabao 2–1 jana Jumapili Oktoba 26, 2025 kuwa sababu ya ukosoaji mkubwa katika mji mkuu wa Uhispania.
Akiwa kwenye matangazo ya moja kwa moja katika mitandao ya kijamii, Yamal alitoa maneno ya kejeli kwa kusema kwamba Real Madrid wanaiba na hulalamika, jambo lililomfanya akabiliane na kelele na matusi kutoka kwa mashabiki wa Santiago Bernabéu wakati Madrid iliposhinda na kuongeza gepu la pointi kutoka mbili hadi tano kileleni mwa La Liga dhidi ya Barcelona.
Wachezaji wa Madrid wakiongozwa na nahodha Dani Carvajal, walimfuata Yamal baada ya kipyenga cha mwisho kupulizwa, wakimkemea kwa maneno kutokana na kauli zake, huku mechi hiyo ikiisha kwa wenyeji kuwa na furaha ya ushindi huo.
Kwa sasa Yamal huenda akawa amejifunza maneno ya kuzungumza kwenye vyombo vya kabla ya mechi ya El Clasico.
Kocha msaidizi wa Barcelona, Marcus Sorg, aliyechukua nafasi ya kocha mkuu Hansi Flick aliyekuwa anatumikia adhabu, amesema mazingira ya uhasama huenda yalichangia kiwango Yamal kuwa chini kwenye mechi hiyo.
“Inawezekana maneno na uhasama uliojengeka kabla ya mechi vilichangia, lakini kwa sababu bado anajifunza kukabiliana na mashabiki, kelele, na mizinga ya uwanjani, atakuwa na jambo la kujifunza siku za usoni. Ni kawaida. Kawaida huwa ana motisha na hucheza vizuri, lakini jana haikuwa rahisi kwake,” amesema Sorg.
Mwaka jana Yamal alikuwa sehemu ya kikosi cha Hispania kilichotwaa ubingwa wa Euro 2024, kisha akatwaa mataji matatu ya ndani na Barcelona, pamoja na kumaliza nafasi ya pili kwenye kura ya Ballon d’Or.
Mshambuliaji huyo kijana amekuwa na tabia ya kutupa vijembe kupitia mitandao ya kijamii, na msimu uliopita alisema kuwa: “Wachezaji wa Real Madrid wanaweza kuongea wakinishinda.”
Msimu uliopita, Barcelona ilishinda El Clásico zote nne, jambo lililowasukuma wachezaji wa Madrid kumkabili kijana huyo, kwenye mechi ya jana Jumapili.
“Maneno ni rahisi,” aliandika Jude Bellingham, kwenye mtandao wa Instagram, akimjibu kwa mafumbo Yamal.