Laliga wabariki ndoa ya Messi

Laliga wabariki ndoa ya Messi

BARCELONA, HISPANIA. CHIFU wa chama cha soka nchini Hispania, ‘LaLiga’ Javier Tebas amesisitiza shirikisho la ligi hiyo limejiandaa vyema kuishi bila ya Lionel Messi na hawana kinyongo juu ya uamisho wake kujiunga na Manchester City katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.

Tebas alisisitiza kuondoka kwa Messi hakuwezi kuwa mwisho wa ligi hiyo licha ya kwamba amekuwa mchezaji aliyeonyesha kiwango kikubwa kuwahi kutokea hapo kabla.

Miongoni mwa mifano aliyoitumia chifu huyo ni namna walivyoweza kuishi bila ya uwepo wa Cristiano Ronaldo na Neymar ambao waliondoka katika nyakati tofauti tofauti lakini LaLiga bado ipo kwenye hadhi kwa sababu walijiandaa vya kutosha kabla ya kuondoka kwao.

“Klabu pekee ambayo pale Ligi Kuu England inayoonekana kuwa kwenye harakati za kuhitaji kumsaini Messi ni Manchester City ambao pia naona wapo nje ya sheria,”

Tebas alisema Man City ineonekana kuwa na nafasi kubwa lakini shaka yake ni kwamba miamba hiyo inaenda nje ya sheria kwa sababu inaonekana kutumia kiasi kikubwa cha pesa tofauti na kile inachoingiza, lakini Man City imeshinda kesi kama hiyo kwenye mahakama ya usuluhishi wa michezo CAS dhidi ya Uefa katika siku za hivi karibuni.

“Sio mimi pekee ambaye nasema jambo hili na sina hofu kuhusu wao lakini mashaka yangu makubwa ni jinsi ambavyo wanafanya mambo haya ya kutumia pesa bila mpangilio tofauti na kile ambacho wanaingiza tena mara kwa mara,”alisema

Hata hivyo Messi kwa upande wake amesema amechoshwa juu ya kile kinachoendelea katika viunga vya Barca kwa sababu yeye ndio anaonekana kuwa sababu ya matatizo yote yanayotokea pale Camp Nou.

“”Ukweli ni kwamba nimechoka kila siku kuwa tatizo kwenye hii klabu,’’alisema Messi.

Hata hivyo Tebas aliongeza hiyo ni sababu mojawapo ambayo inamfanya aamini timu hiyo ina nafasi kubwa ya kuipata saini ya Messi ambaye mkataba wake unatarajiwa kuisha mwisho wa msimu.