LaLiga, Bundesliga kote ni moto
Muktasari:
- Huko kwenye La Liga, shughuli ilianzia Ijumaa, lakini kasheshe kubwa lipo Jumamosi, ambapo Barcelona itakuwa nyumbani kucheza na Athletic Bilbao, huku Osasuna ikicheza na Real Sociedad, Alaves na Celta Vigo na Villarreal kumenyana na Mallorca.
MADRID, HISPANIA: MAMBO ni moto. Ndicho unachoweza kusema kuhusu kurejea upya kwa ligi mbalimbali za Ulaya, ambapo kote kutakuwa na kasheshe kubwa kuanzia kwenye La Liga, Bundesliga, Ligue 1 na Serie A, kati ya Ligi Kuu tano bora za Ulaya.
Huko kwenye La Liga, shughuli ilianzia Ijumaa, lakini kasheshe kubwa lipo Jumamosi, ambapo Barcelona itakuwa nyumbani kucheza na Athletic Bilbao, huku Osasuna ikicheza na Real Sociedad, Alaves na Celta Vigo na Villarreal kumenyana na Mallorca.
Jumapili, vinara Real Madrid watakuwa ugenini kucheza na Elche, wakati Oviedo itakipiga na Rayo Vallecano, Real Betis na Girona na Getafe itakuwa na shughuli pevu mbele ya Atletico Madrid.
Kwenye Bundesliga, Jumapili kutakuwa na mechi mbili tu, RB Leipzig ikiwa nyumbani kucheza na Werder Bremen, wakati St Pauli itakipiga na Union Berlin, lakini kazi nzito ni Jumamosi, ambapo Beyern Munich itakuwa Allianz Arena kucheza na Freiburg, huku Borussia Dortmund ikicheza na VfB Stuttgart, FC Heidenheim na Borussia Monchengladbach, huku Wolfsburg ikikipiga na Bayer Leverkusen, FC Cologne na Eintracht Frankfurt na Augsburg watacheza na Hamburger SV.
Huko kwenye Serie A, mambo ni matata, ambapo Jumamosi kutakuwa na mechi nne, Cagliari ikikipiga na Genoa, Udinese na Bologna, wakati Fiorentina itaonyeshana ubabe na Juventus, huku Napoli ikiwa na kasheshe zito mbele ya Atalanta.
Kwa Jumapili, shida inaendelea, lakini kasheshe zito litakuwa kwenye Milan derby, wakati Inter Milan itakapokipiga na AC Milan uwanjani San Siro, huku Hellas Verona ikicheza na Parma, Cremonese na AS Roma na Lazio zitaonyeshana ubabe na Lecce.
Kwenye Ligue 1, Jumapili Auxerre itakuwa nyumbani kuikaribisha Lyon, wakati Brest ilikuwa na kazi pevu mbele ya Metz, huku Nantes ikikipiga na Loriente, Toulouse na Angers na Lille itakuwa na kipute cha maana dhidi ya Paris FC.
Kwa Jumamosi kutakuwa na mechi tatu tu, ambapo Lens itakuwa nyumbani kucheza na Strasbourg, huku Rennes ikicheza na AS Monaco na mabingwa watetezi Paris Saint-Germain watakuwa uwanjani kwao Parc des Princes kucheza na Le Havre. Mambo ni moto.