Nawakumbusha tu Eden Hazard ana umri wa miaka 34
Muktasari:
- Alikuwa bonge la mchezaji. Alikuwa na kitu kinaitwa ulimbo katika miguu yake. Alikuwa akiuweka mpira katika mpira miguu yake unanasa na kutulia. Alikuwa akiamua kuteleza katikati ya mabeki anaweza kufanya hivyo kadri ajisikiavyo.
EDEN Michael Walter Lucien Hazard tulipenda kumuita Eden Hazard kumbe ana umri wa miaka 34 tu. Nimeamua kuwakumbusha. Unaweza kuendelea na maisha yako ukadhani kwamba labda alistaafu mpira wa miguu enzi ambazo kina Zinedine Zidane na Ronaldo De Lima walistaafu soka kumbe wala sio hivyo.
Alikuwa bonge la mchezaji. Alikuwa na kitu kinaitwa ulimbo katika miguu yake. Alikuwa akiuweka mpira katika mpira miguu yake unanasa na kutulia. Alikuwa akiamua kuteleza katikati ya mabeki anaweza kufanya hivyo kadri ajisikiavyo.
Hazard alikuwa kama Kevin De Bruyne au Son Heung-Min. Wale wachezaji ambao walikuwa hawachezaji katika timu zenye mashabiki wengi huku kwetu Afrika lakini kila mmoja aliwapenda na kukiri vipaji vyao. Na kila mmoja akatamani kwamba wangecheza katika klabu yake.
Kwanza walikuwa wana vipaji maridadi lakini pili walikuwa sio wachezaji wakorofi. Muda wote wangekuacha mdomo wazi kwa uwezo wao na hawakukupa sababu hata moja ya kuwachukia. Wakati wenzake wakiendelea kucheza, Eden yeye amestaafu na amesahau kucheza mpira.
Nimemkumbuka Eden wakati huu Ligi mbalimbali zikisonga mbele duniani kote. Nimekumbuka kwamba ana umri wa miaka 34 tu. unaweza kudhani kwamba Hazard yupo sehemu akiwa mzee kumbe yupo sehemu akinywa bia zake tu na kutazamana watu wengine wakiwa wanakanyagana uwanjani.
Huwa namkumbuka Hazard na kisha naishia kucheka. Wakati yeye akiwa na umri wa miaka 34 kumbe Cristiano Ronaldo anakusanya pesa za waarabu huku akiwa na miaka 40. Wakati Hazard akiwa na miaka 34 kumbe Luka Modric ana umri wa miaka 40 na anacheza Ligi kuu ya Italia akiwa na miaka 40. Serie A ni miongoni mwa ligi kuu tano barani Ulaya.
Wakati Hazard akiwa anakunywa bia zake mahala kumbe Lionel Messi ana umri wa miaka 38 na anacheza Ligi Kuu ya Marekani. Wakati huo huo, Sergio Ramos ana miaka 39 anacheza klabu ya Monterrey ya Ligi Kuu ya Mexico.
Kuna rundo la wachezaji wengi waliompita umri kwa mbali ambao bado wanacheza soka la kishindani. Hazard ameishia zake njiani na wengi wanaweza kuniambia kwamba ni kwa sababu ya majeraha. Naweza kukubali lakini kumbe yeye mwenyewe alikuwa anasubiri kustaafu kwa hamu kubwa.
Kuna mambo mawili hapa. Kwanza kabisa ni kwamba kuna orodha ya wachezaji kadhaa ambao maisha yao yalibadilika pale walipoamua kubadili hali ya hewa. Hazard anaingia katika kundi hili. Maisha yalikuwa matamu mpaka pale alipowaambia Chelsea kwamba ilikuwa imetosha kucheza timu yao na alikuwa anataka kwenda Real Madrid.
Inakuwa ngumu kumzuia mchezaji wa namna hii. Ni kama ambavyo Philippe Coutinho alipowaambia Liverpool kwamba ilikuwa basi kwake kucheza Anfield na alikuwa anataka kwenda Nou Camp kucheza Barcelona. Liverpool pia walikuwa na mkosi huu mapema tu wakati Fernando Torres alipowaambia basi kucheza Anfield na alikuwa anataka kucheza Stamford Bridge.
Wote hawa maisha yao hayakuendelea kuwa yale yale. Ni kama kilichomtokea Hazard alipoamua kuwapa mkono Chelsea kwenda Real Madrid kucheza dimba la Santiago Bernabeu. Tatizo nimemkumbuka Hazard kwa sababu mbili tofauti.
Kwanza ni namna ambavyo alipokea kwa shangwe kustaafu kwake. Sidhani kama alipambana sana kuendelea kuwepo uwanjani kuitumikia Real Madrid licha ya changamoto za hapa na pale. Baada ya kutangaza kustaafu kucheza soka mwaka 2023 alisikika akisema “KIdogo kidogo ni muda wa kufurahia maisha na familia na marafiki. Kunywa bia za Jupiler na marafiki.”. Jupiler ni bia maarufu nchini Ubelgiji.
Baadaye Hazard alianza kunenepa na mwisho alisikika akidai kwamba angependa kupunguza pombe pamoja na nyama choma. Wakati huo huo alielezea jinsi ambavyo mpira, hasa Ligi kuu ya England, vilikuwa vinamnyima uhuru wa kula maisha.
Kitu ambacho kilinifanya nimuelewe zaidi na maisha yake ni kwamba kumbe na yeye alikuwa ni Ronaldinho mwingine tu. Alikuwa ni Ronaldo de Lima mwingine tu katika namna ambavyo alikuwa anayafikiria maisha. Katika mahojiano yake fulani alielezea namna ambavyo hata mpira wenyewe alikuwa anautazama katika namna tofauti na sisi ambavyo tulikuwa tunautazama.
Aliwahi kunukuliwa mahala akidai kwamba kwake kupiga pasi ya mwisho ya bao au kufunga bao havikuwa vitu muhimu kuliko kuuchezea mpira wenyewe. Huyu ndio aina ya wachezaji wa Kibrazil lakini ambao kwa bahati mbaya walizaliwa Ubelgiji.
Kuna wachezaji ambao wanajitunza na kulijinda na kuutamani mpira. Kila nilipomfuatilia Eden hazard niligundua kwamba kumbe hakuwa mchezaji wa namna hiyo. Ndio maana hakuona shida sana kuamua kustaafu mpira akiwa na umri wa miaka 32 tu.
Imepita miaka miwili sasa tangu astaafu soka na wakati huu ambao ligi mbalimbali zimeanza kupamba moto barani Ulaya kama ingekuwa nyakati zile basi Hazard angekuwa mchezaji ambaye anatupa tumbo joto.
Vipaji vinaendelea kupungua katika ligi mbalimbali za Ulaya huku kukiwa na wachezaji ambao wameamua kujiizesha tu kwa ajili ya kula bia. Unapokumbuka kwamba Hazard na Granit Xhaka wamepishana mwaka mmoja tu unajikuta umeishiwa pawa. Kumbe kama angekuwa amedhamiria kupambana na majeraha yake na kuachana na pombe si ajabu angekuwa bado yupo uwanjani kwa sasa akisakata soka. inawezekana isingekuwa Ligi kuu ya England lakini kumbe angeweza kuwa mahala.
Na wakati ule anastaafu angeweza kujaribu kujikaza kadri awezavyo ili awe uwanjani walau akila pesa za Waarabu kumbe mwenzetu alikuwa anawaza kustaafu tu ili anywe pombe na ndugu, jamaa na marafiki. Wakati mwingine maisha ndivyo yalivyo.