La Liga mambo ni moto

MAMBO ni moto huko kwenye mchakamchaka wa La Liga. Barcelona itakuwa kwenye kasheshe zito la kuwakabili Athletic Bilbao ugenini, sawa na mahasimu wao Real Madrid ambao pia watakuwa ugenini kukipiga na wababe wa zamani, Valencia.
Mbio za kusaka ubingwa wa La Liga katika msimu huu wa 2023/24 zimezidi kunoga, huku wikiendi hii ya wiki ya 27 ya mechi za michuano hiyo, ikitarajia kuwapa burudani ya kutosha mashabiki wake kutokana na utamu wa mechi zilizopo.
Jana Ijumaa kulikuwa na kipute kimoja tu huko Celta Vigo na iliichapa bao 1-0 Almeria, shukrani kwa bao la Oscar Mingueza la dakika ya 73, lililoipeleka hadi nafasi ya 16 na pointi 24 huku Almeria ikiendelea kuburuza mkia na pointi zao 9 baada ya zote kucheza mechi 27.
Hata hivyo, uhondo wa mikikimikiki hiyo utaendelea tena leo Jumamosi na kesho Jumapili kwa mechi kali kabisa zenye ushindani mkalio.
Mechi ya kwanza kabisa leo, Sevilla itakuwa na kigumu mbele ya Real Sociedad. Sevilla itakosa mastaa wake kadhaa wakiwamo Lucas Ocampos na Djibril Sow, jambo ambalo litamfanya kocha Quique Sanchez Flores kufanya mabadiliko kwenye kikosi chake kutoka kile kilichochapwa 1-0 na Real Madrid. Bila shaka atakwenda na mfumo wa 3-5-2, ambapo Isaac Romero na Youssef En-Nesyri wataongoza safu ya ushambuliaji.
Real Sociedad iliyotupwa nje kwenye Copa del Rey kwa mikwaju ya penalti mbele ya Mallorca huku ikitambua Jumanne itakuwa na mechi ngumu dhidi ya Paris Saint-Germain kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, bila ya shaka itafanya mabadiliko makubwa ya kikosi chake. Ngoja tuone itakavyokuwa.
Rayo Vallecano itakuwa na kibarua mbele ya Cadiz. Rayo ilikumbana na kipigo kizito kutoka kwa Girona kwenye mchezo uliopita, lakini imepambana kupata walau pointi moja kwenye mechi mbili zilizopita wakiwa chini ya kocha mpya Inigo Perez.
Cadiz wao walicheza kwa kiwango kizuri sana katika mchezo uliopita dhidi ya Celta, ilifunga bao lake la kwanza tangu Mauricio Pellegrino alipochukua mikoba kwenye sare ya 2-2. Darwin Machis huenda akaanza katika mchezo huo.
Getafe na Las Palmas ni vuta nikuvuta. Miamba Getafe haitakuwa na huduma ya mabeki Djene na Omar Alderete, lakini baada ya kuchapwa 4-0 na Barcelona kwenye mechi iliyopita, bila shaka wataingia uwanjani kuwakabili Las Palmas wakiwa na hasira kubwa.
Las Palmas nao watakosa huduma za mastaa wao kadhaa akiwamo Alex Suarez, hivyo kutakuwa na mabadiliko kwenye kikosi huku Julian Araujo na Marvin Park wakitazamiwa kuwa chaguo kwenye beki ya kulia. Sandro na Munir wanaweza kuanza.
Mashabiki wengi watasubiri kuona kile kitakachokwenda kutokea kwenye mchezo wa Valencia na Real Madrid. Kocha wa Valencia, Ruben Baraja atakuwa na nafasi ya kupanga kikosi chake kikali zaidi katika mchezo huo, huku Real Madrid wakitambua wiki ijayo watakuwa na kazi nzito dhidi ya RB Leipzig kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, hivyo kocha Carlo Ancelotti atakabiliana na mechi hiyo kwa akili nyingi. Joselu hana uhakika wa kuwamo kwenye mchezo huo, lakini Antonio Rudiger anatazamiwa kurejea.
Kesho, Jumapili shughuli nzito itaendelea na Villarreal itakipiga na Granada. Villarreal ilishinda ugenini dhidi ya Real Sociedad kwenye mechi iliyopita, lakini wataingia kwenye mechi hiyo wakiwa na kazi nzito kwenye safu ya ulinzi, kama ilivyo kwa Granada, ambao watamkosa Jorge Cuenca. Granada ilibadilika kimtindo na katika mechi tatu zilizopita ilifanikiwa kutoa sare.
Kocha Diego Simeone na chama lake la Atletico Madrid litakuwa na shughuli pevu mbele ya Real Betis.
Atletico Madrid ilikumbana na kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Athletic Bilbao kwenye mchezo wa pili wa nusu fainali ya Copa del Rey juzi Alhamisi, hivyo itahitaji kupata matokeo chanya katika mchezo huo wa La Liga kwenye kipute dhidi ya Betis. Antoine Griezmann hakucheza mechi iliyopita na bila shaka anaweza kuungana na Memphis Depay na Alvaro Morata kwenye safu ya ushambuliaji.
Betis imekuwa na majeruhi kadhaa kwenye kikosi chao, lakini bado iliweza kuishinda Bilbao katika mchezo uliopita. Hata hivyo, kuna wasiwasi wakakosa huduma ya staa wao matata kabisa Nabil Fekir.
Mallorca na Girona watamaliza ubishi, huku mchezo huo ukitarajiwa kuwa na upinzani mkali. Mallorca wanafahamu kile ambacho watapaswa kufanya kwenye mechi hiyo, lakini Girona wanafukuzia nafasi ya kucheza michuano ya Ulaya msimu ujao. Mastaa wao walikuwa majeruhi akiwamo Daley Blind wanatarajia kurejea kwenye mchezo huo.
Mchezo wa mwisho kwa siku ya kesho, utawahusu Bilbao na Barcelona huko San Mames. Bilbao itakuwa na mechi nyingine ngumu ndani ya siku nne tu baada ya kuwachapa Atletico kwenye nusu fainali ya Copa del Rey. Itakosa wachezaji wake wawili matata kabisa, Nico Williams na Dani Vivian wanaotumikia adhabu ya kadi, huku Alex Berenguer na Yeray wanatazamiwa kuanza.
Barcelona wachezaji wao wote hasa kwenye safu ya ushambuliaji wapo fiti na jambo hilo linampa wakati mgumu kocha Xavi katika uteuzi wa kikosi chake.
Jumatatu kutakuwa na mchezo mmoja na Osasuna watacheza na Alaves. Katika mchezo huo, tatizo la Osasuna olitakuwa kwa mastaa wake Ante Budimir, Jose Arnaiz na Raul Garcia ambao wote wana hatihati, lakini wapinzani wao Alaves wao waliopoteza mechi moja tu kati ya nane zilizopita walicheza kwenye ligi katika mwaka huu, watakosa Aleksandar Sedlar, hivyo kufanya mechi hiyo kutarajiwa kuwa na upinzani mkali ndani ya uwanja.