Kweli Gyokeres anaitaka Arsenal

Muktasari:
- Hilo limekuja baada ya kuwasili kwa kiungo Martin Zubimendi kwenye kikosi hicho cha Emirates.
LONDON, ENGLAND: ARSENAL ipo kwenye hatua za mwisho kabisa za kukamilisha usajili wao wa pili dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi baada ya chama hilo linalonolewa na Mhispaniola Mikel Arteta kuwa kwenye wakati mzuri wa kunasa huduma ya straika wa Sporting CP, Viktor Gyokeres.
Hilo limekuja baada ya kuwasili kwa kiungo Martin Zubimendi kwenye kikosi hicho cha Emirates.
Gyokeres alikuwa kwenye rada za timu nyingi kama Liverpool, Chelsea na Manchester United, lakini kinachoonekana kwenda kutokea ni kwamba staa huyo ataondoka Lisbon ili kutua London.
Gyokeres ni miongoni mwa mastraika bora kabisa duniani kwa sasa baada ya kufunga mabao 97 katika mechi 102 alizocheza kwenye kikosi cha Sporting.
Sasa kinachoelezwa ni kwamba straika Gyokeres yupo tayari hata kupoteza pesa zake ili tu kufanikisha dili hilo la kwenda kujiunga na Arsenal baada ya miamba hiyo ya Emirates ikiwa bado haijafikiana juu ya ada ya uhamisho wa mshambuliaji huyo.
Sporting inahitaji Pauni 68.5 milioni ili kufanya dili hilo kukamilika na Gyokeres, sasa yupo tayari kujitolea sehemu ya mkwanja wake ili kufanya hilo litokee. Na kwa mujibu wa Fabrizio Romano, Gyokeres yupo tayari kujitolea Pauni 1.73 milioni ili kufanya uhamisho huo kutokea, akatue Arsenal.