Kwa mziki huu wa Spurs, mtakoma
Muktasari:
- Kocha mpya wa Spurs, Thomas Frank anafanya usajili wa wachezaji wakubwa sokoni ikiwa ni sehemu ya kukiandaa kikosi hicho kisirudia mambo ya msimu uliopita, wakati ilipomaliza nafasi ya 17 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England.
LONDON, ENGLAND: TOTTENHAM Hotspur sasa imewasha moto dirisha hili la usajili, ikinyakua huduma ya winga wa West Ham United, Mohammed Kudus kwa Pauni 55 milioni na sasa inakaribia kwenye kunyakua saini ya kiungo wa Nottingham Forest, Morgan Gibbs-White, ambaye anawagharimu Pauni 60 milioni.
Kocha mpya wa Spurs, Thomas Frank anafanya usajili wa wachezaji wakubwa sokoni ikiwa ni sehemu ya kukiandaa kikosi hicho kisirudia mambo ya msimu uliopita, wakati ilipomaliza nafasi ya 17 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England.
Spurs ilifanya hovyo chini ya Kocha Ange Postecoglou, lakini ilifanikiwa kunasa taji la Europa League, lililowapa tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, huku likiwavutia wachezaji wengi kushawishika kwenda kujiunga na kikosi hicho cha London Kaskazini.
Kutokana na hilo, hadi sasa Spurs imeshakamilisha usajili wa wachezaji wanne, huku Kocha Frank akiendelea kupambana kutengeneza timu itakayokuwa moto msimu ujao.
Spurs inapambana pia kunasa huduma ya fowadi wa Brentford, timu ya zamani ya kocha Frank, Yoane Wissa ili aje kukipiga kwenye hiyo, huku ikiandaliwa ada ya Pauni 50 milioni kumnasa.
Kama wachezaji wote wanaosakwa Spurs wakipatikana, basi Frank atakuwa ameunda timu matata kabisa na golini atakuwa Vicario na atalindwa na mabeki Pedro Porro, upande wa kulia, Destiny Udogie kushoto na mabeki wa kati ni Cristian Romero na Mickey van de Ven.
Kwenye kiungo, kocha Frank atakuwa na huduma za mastaa Rodrigo Bentancur na Lucas Bergvall na Morgan Gibbs-White huku Yves Bissouma na Pape Sarr watasubiri benchi.
Spurs inahusishwa pia na mpango wa kumsajili staa Adam Wharton, ambaye mashabiki wake wanaamini ni Namba 6 bora kabisa, huku kwenye safu ya ushambuliaji Mathys Tel, Wissa na Kudus, huku mastaa kama Brennan Johnson, Dejan Kulusevski, James Maddison, Son Heung-min na Wilson Odobert waraendelea kusubiri kwenye benchi sambamba na Dominic Solanke.