Kutoka safari ya ubingwa wa EPL hadi giza la Championship
Muktasari:
- Kwa sasa ipo nafasi ya pili kutoka mkiani, ikiwa tofauti ya pointi nane dhidi ya West Bromwich Albion na Blackburn Rovers zilizoko nafasi ya kukwepa kushuka daraja.
LEICESTER, ENGLAND: UNAIKUMBUKA Leicester City ya kiumeni iliyobeba ubingwa wa Ligi Kuu England mwaka 2015/16, golini Kasper Schmeichel, hapa Robert Huth, pale Wes Morgan, katikati Danny Drinkwater, N'golo Kante, pembeni Riyard Mahrez, mbele Jamie Vardy? ndio. Kwa sasa hali yao ni mbaya, hawatamaniki na wapo karibu kushuka, kwenda Ligi Daraja lapili.
Baada ya wikiendi kupoteza mechi yao dhidi ya Portsmouth ni rasmi sasa wababe hao wa zamani wa EPL wanatakiwa walau kushinda mechi zao zote ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kubakia Ligi Daraja la kwanza.
Kwa sasa ipo nafasi ya pili kutoka mkiani, ikiwa tofauti ya pointi nane dhidi ya West Bromwich Albion na Blackburn Rovers zilizoko nafasi ya kukwepa kushuka daraja.
Kwa sasa kuna mwanga mdogo wa matumaini kwa Leicester, kwani West Brom inaweza kukatwa pointi kati ya mbili hadi nne kwa madai ya kukiuka sheria za masuala ya kifedha ingawa hata hilo likitokea bado Leicester itakuwa na kazi kubwa ya kufanya.
Kiujumla zimebakia mechi tatu tu za kuwawezesha kujinasua na hatari ya kushuka daraja na baada ya mechi ya wikiendi iliyopita sasa itacheza nyumbani dhidi ya Hull City yenye njaa na baadae pia itaikaribisha Millwall kabla ya kumalizia msimu ugenini dhidi ya Blackburn Rovers ambao pia wanapambana kujinusuru.
Moja kati ya sababu zinazotajwa kuchangia anguko la wababe hawa kwanza ni kifo cha aliyekuwa mmiliki wao mwenyekiti Vichai Srivaddhanaprabha aliyefariki dunia mwaka 2018 kutokana na ajali ya helikopta nje ya uwanja wa King Power.
klabu ilimpoteza mtu aliyebadilisha kabisa Leicester kutoka kuwa timu ya kawaida ya katikati ya jedwali la Championship hadi kuwa mabingwa wa Ligi Kuu England.
Mtoto wake Aiyawatt Srivaddhanaprabha haonekani kuwa na hali ya kujitoa na ufahamu mzuri wa mpira wa miguu kama ilivyokuwa kwa baba yake.
Vilevile, klabu hiyo kwa sasa inakumbana na changamoto ya masuala ya kifedha wakiwa wanaandamwa na madeni makubwa yaliyosababishwa na kuyumba kwa kampuni ya King Power ambayo ndio inaimiliki.
Mbali ya hilo, pia inaelezwa mfumo wa namna timu inajiendesha umebadilika sana kiasi cha kusababisha watumie pesa nyingi katika kusajili wachezaji wapya.
Zamani chini ya skauti Steve Walsh klabu ilifanikiwa kusajili mastaa kama Jamie Vardy, N’Golo Kante na Riyad Mahrez kwa kiasi kiduchu sana cha pesa kisha baadae wakaenda kuisaidia timu na kuuzwa kwa bei mbaya.
Tangu Walsh aondoke timu hiyo imekuwa ikitumia sana pesa kusajili na mwishowe imeshindwa kupata ubora sawa na ule ambao ulikuwepo kwa wakati huo.