City vs Arsenal, mechi kubwa ya kuamua ubingwa EPL
Muktasari:
- Hilo ni wazo linalofanana na michezo ya Marekani, lakini pia limeanza kutumika katika baadhi ya ligi za Ulaya kama Ubelgiji, Ugiriki na Scotland. Kwa mfano, pambano la kusisimua la timu tatu la kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Scotland linaelekea mwisho wake huku Heart of Midlothian ikikutana na Hibernian, Rangers na Motherwell, Falkirk na Celtic ndani ya wiki tatu.
LONDON, ENGLAND: MARA kwa mara, baadhi ya wataalamu wa masoko ya michezo wamekuwa wakishauri klabu za Ligi Kuu kuzingatia mfumo wa mchujo mwishoni mwa msimu. Wazo hilo halijawahi kufanikiwa, lakini dhana yake ni kwamba msimamo wa ligi ‘ugawanyike’ mwishoni mwa msimu ili kuruhusu mfululizo mfupi wa mechi zenye ushindani mkali zaidi juu na chini ya jedwali, na kuongeza msisimko.
Hilo ni wazo linalofanana na michezo ya Marekani, lakini pia limeanza kutumika katika baadhi ya ligi za Ulaya kama Ubelgiji, Ugiriki na Scotland. Kwa mfano, pambano la kusisimua la timu tatu la kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Scotland linaelekea mwisho wake huku Heart of Midlothian ikikutana na Hibernian, Rangers na Motherwell, Falkirk na Celtic ndani ya wiki tatu.
Hata hivyo, hakujawahi kuwa na hamasa kubwa ya kuanzisha mfumo huo katika Ligi Kuu England. Ratiba ya ligi hiyo tayari inaonekana imesongamana sana na mfumo wa kawaida wa kucheza nyumbani na ugenini umeonekana kuwa bora tangu kuanzishwa kwa ligi ya soka 1888.
HAKUNA TATIZO,
HAKUNA KUBADILI
Mfumo huo wa jadi unaleta usawa, uthabiti na uenedelevu ambapo kila mechi ina thamani sawa katika Ligi Kuu England. Lakini jambo ambalo hutokea mara chache ni pambano la ubingwa lenye uzito mkubwa kama lile la Manchester City na Arsenal, Jumapili hii.
Tovuti ya Ligi Kuu inaelezea mechi hiyo inayopigwa Etihad kama “mechi kubwa zaidi kwa miaka mingi”, kauli inayoungwa mkono na mshambuliaji wa zamani wa Liverpool, Michael Owen, aliyesema kuwa ushindi utamsukuma mshindi karibu na ubingwa.
Beki wa zamani wa Manchester United, Gary Neville, anaiita mechi hiyo “kubwa sana” na “ya kihistoria” ambayo itaamua msimu wa Ligi Kuu England. Ni vigumu kupingana nao.
Katika vyombo vya habari vya michezo mara nyingi kunakuwa na matumizi ya lugha ya kupitiliza. Siyo kila mechi kubwa huwa na uzito unaosemwa. Katika msimu mmoja wa Ligi Kuu England kuna mechi 380, lakini ni chache zinazoweza kuitwa za kuamua msimu.
Mara ya mwisho kuona mechi ya kuamua ubingwa moja kwa moja ilikuwa msimu wa 1988-89, wakati Arsenal ilipocheza na Liverpool katika mechi ya mwisho wa msimu. Arsenal ilihitaji ushindi wa mabao mawili na ilifanikiwa dakika za mwisho kupitia bao la Michael Thomas na kutwaa ubingwa huo.
Katika enzi ya Ligi Kuu England (miaka 33 iliyopita), ni mara chache sana timu za nafasi ya kwanza na ya pili zimekutana mwishoni mwa msimu zikiwa na tofauti ndogo ya pointi kama sasa. Kwa hakika, hali kama hiyo imetokea mara saba tu.
Hata baadhi ya matukio hayo yanaweza kujadiliwa, lakini ujumbe ni kwamba hali kama hiyo ni nadra sana. Ubingwa hautaamuliwa Jumapili, lakini mechi hii ni muhimu sana. Ikiwa Manchester City itashinda itakuwa pointi tatu tu nyuma ya Arsenal ikiwa na mechi mkononi. Sare itaiweka Arsenal mbele kwa pointi sita. Ushindi wa Arsenal utaifanya iongoze kwa pointi tisa na kuwa karibu sana na ubingwa.
Historia inaonyesha umuhimu wa mechi kama hizi kwani 2002, Arsenal iliishinda Manchester United na kutwaa ubingwa huku 2003 Manchester United ilipata sare na baadaye kushinda ubingwa. Lakini, 2008, Manchester United ilishinda ubingwa licha ya shinikizo na ushindani mkali, ilhali
2010 Chelsea ilishinda na kutwaa ubingwa. Vivyo hivyo 2012, Manchester City ilishinda na kuchukua ubingwa kwa tofauti ya mabao na 2014 Manchester City ilibeba ubingwa baada ya Liverpool kupoteza mwelekeo, na ni 2023 ambapo Manchester City iliifunga Arsenal na kuchukua ubingwa mapema.
Mojawapo ya mechi muhimu zaidi ilikuwa Dabi ya Manchester 2012, ambapo ushindi wa Manchester City uliweka msingi wa kutwaa ubingwa.
Kwa kawaida, timu yenye mwendelezo mzuri wa matokeo ndiyo hushinda mechi hizi muhimu. Hii inaweza kuwa habari mbaya kwa Arsenal kutokana na mabadiliko ya hali ya mchezo na matokeo ya hivi karibuni.
Mwezi mmoja uliopita, Arsenal ilikuwa inaongoza kwa pointi tisa, lakini ushindi wa Manchester City katika fainali ya Kombe la Carabao uliwapa nguvu mpya na kuiweka Arsenal kwenye wakati mgumu. Katika wiki za karibuni, mitazamo kuhusu timu hizo mbili imebadilika, ingawa Arsenal ilikuwa ikisifiwa kwa uthabiti wa msimu mzima.
Swali ni kama mechi ya leo, Jumapili, itaendana na mwenendo wa wiki za hivi karibuni au ule wa miezi saba ya kwanza ya msimu? Historia inaonyesha kuwa mwendelezo wa karibuni huwa na uzito mkubwa kuliko historia ya muda mrefu. Kwa Arsenal, kupata ushindi au hata sare katika mechi hiyo kutakuwa na maana kubwa sana. Lakini kama Manchester City itashinda hali inaweza kuwa ngumu zaidi kwa Arsenal kuliko inavyoonekana kwenye jedwali. Bado kutakuwa na mechi kadhaa za kucheza, na msimu huu umeonyesha kuwa kunaweza kuwa na mabadiliko mengi hadi mwisho.
Hata hivyo, hakuna shaka mechi ya leo ni kubwa sana. Kwa Manchester City, wanataka kurejesha ubingwa walioupoteza kwa Liverpool msimu uliopita, huku kukiwa na shaka kuhusu mustakabali wa Pep Guardiola na masuala ya kisheria yanayoikabili klabu hiyo juu ya masuala ya matumizi ya fedha katika uendeshaji wa klabu.