Kumbe Rooney ana siri ya ushindi wa Man United

Muktasari:
Rooney, ambaye ni nahodha wa kikosi cha Manchester United aliwakusanya wenzake kwenye vyumba vya kubadilishia nguo Uwanjani Old Trafford na kuwaambia kwamba wasahau kitendo cha kufungwa na Arsenal kwenye Kombe la FA na kwamba ni lazima waichape Spurs.
KOCHA, Louis van Gaal amefichua kwamba Wayne Rooney alitumia dakika kadhaa kuzungumza na wachezaji kabla ya mchezo wao dhidi ya Tottenham Hotspur juzi Jumapili, lakini akampigia saluti Maroane Fellaini kwamba ni kiboko.
Rooney, ambaye ni nahodha wa kikosi cha Manchester United aliwakusanya wenzake kwenye vyumba vya kubadilishia nguo Uwanjani Old Trafford na kuwaambia kwamba wasahau kitendo cha kufungwa na Arsenal kwenye Kombe la FA na kwamba ni lazima waichape Spurs.
Man United ilishuka uwanjani na kuichapa Spurs mabao 3-0 na hivyo kujiweka kwenye nafasi nzuri kwenye Ligi Kuu, lakini Van Gaal amesema Fellaini na kiungo Michael Carrick walionyesha tofauti kubwa katika mchezo huo.
Van Gaal alisema Carrick aliwamaliza Spurs kwa pasi zake kali ikiwamo ya bao la kwanza lililofungwa na Fellaini, ambaye alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo.
“Michael Carrick si tu nahodha msaidizi, ana pasi za hatari, anapiga pande zote hasa pasi za mbele. Tunahitaji viungo wa pasi kama hizo,” alisema Van Gaal.
Kwenye mchezo huo, Fellaini aligusa mpira mara 56, lakini Juan Mata aliyekuwa kwenye ubora wake kabla ya kutolewa aligusa mpira mara 61.
Mata alielewana vizuri na Ander Herrera na Antonio Valencia na kuonyesha kiwango kikubwa ndani ya uwanja na kuwafanya mashabiki waliofika Uwanjani Old Trafford kusimama kumpigia makofi wakati alipokuwa anatoka kama walivyofanya kwa Fellaini, ambaye alikuwa na msaada mkubwa sana katika ushindi huo muhimu.
Kiwango cha Mata kimeanza kumpasua kichwa kocha Van Gaal juu ya upangaji wa kikosi chake katika mchezo ujao dhidi ya Liverpool Uwanjani Anfield kwa sababu Angel Di Maria atakuwa amemaliza adhabu yake iliyomfanya akose mechi ya Spurs.
Uwepo wa Carrick uliifanya Man United kupunguza tatizo la kupiga pasi za nyuma, ambazo zilionekana kuwa tatizo katika mechi za karibuni ikiwamo ya kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Arsenal kwenye Uwanjani wa Old Trafford wiki iliyopita.
Kwa matokeo hayo Man United sasa imefikisha pointi 56, nane nyuma ya vinara Chelsea huku ligi ikiwa imebakiza mechi tisa kufika ukingoni.