Emiliano atoa msimamo ishu ya Man United

Muktasari:
- Martinez ambaye alihamia Aston Villa kutoka Arsenal 2020 ameibuka kuwa mmoja wa makipa bora duniani akiwika Ligi Kuu England na pia kuisaidia Argentina kutwaa Kombe la Dunia 2022.
BIRMINGHAM, ENGLAND: KIPA wa Aston Villa, Emiliano Martinez amevunja ukimya kuhusu hatima yake huku tetesi za kujiunga na Manchester United zikishika kasi.
Martinez ambaye alihamia Aston Villa kutoka Arsenal 2020 ameibuka kuwa mmoja wa makipa bora duniani akiwika Ligi Kuu England na pia kuisaidia Argentina kutwaa Kombe la Dunia 2022.
Kutokana na mafanikio hayo, kipa huyo mara kwa mara ameendelea kuhusishwa na timu kubwa, lakini uwezekano wa nyota huyo mwenye umri wa miaka 32 kuondoka Villa haujawahi kuwa mkubwa kama sasa.
Martinez alionekana kuwaaga mashabiki wa Aston Villa baada ya mechi ya ligi dhidi ya Tottenham Hotspur huku tetesi zikimhusisha na Manchester United na Barcelona. Hata hivyo, Barcelona imeripotiwa kutaka kumsajili kipa wa Espanyol, Joan Garcia, hivyo ni Man United inaonekana peke yake dhidi Martinez.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kujiunga na timu ya taifa, Martinez alisema: “Mustakabali wangu? Siujui kwa kweli. Nimekuja hapa kuchezea timu ya taifa na hilo ndilo jambo pekee linalonihusu kwa sasa.
“Je nataka kujiunga na klabu nyingine? Dirisha la usajili ndiyo kwanza limefunguliwa kwa hiyo bado kuna muda mrefu mbele yetu.”
Kwa sasa, Martinez anajikita kwenye mechi zijazo za kufuzu Kombe la Dunia akiiwakilisha Argentina ingawa mabingwa hao watetezi tayari wamefuzu 2026.
Argentina inatarajiwa kucheza dhidi ya Chile na Colombia.