Kumbe Paul Pogba bado pesa ipo
Muktasari:
- Makala hii inaangazia kwa kina utajiri wa Paul Pogba kuanzia mali anazomiliki, mikataba yake ya kibiashara, msaada kwa jamii, hadi maisha yake binafsi.
MONACO, UFARANSA: LICHA ya kukumbwa na kashfa nzito za kufungiwa kucheza soka kwa muda wa miaka minne na baadaye adhabu hiyo kupunguzwa kufikia miezi 18, kutokana na matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku (doping), Paul Pogba bado anaendelea kuwa miongoni mwa wanasoka matajiri.
Makala hii inaangazia kwa kina utajiri wa Paul Pogba kuanzia mali anazomiliki, mikataba yake ya kibiashara, msaada kwa jamii, hadi maisha yake binafsi.
ANAPIGAJE PESA
LICHA ya kuwa nje ya ajira kwa muda mrefu, kwa mujibu wa tovuti ya Celebrity networth utajiri wa staa huyu hadi sasa unafikia dola 100 milioni.
Utajiri huo unatokana na mshahara na madili mengine ya nje ya uwanja aliyowahi kuyapata hapo awali. Kwa sasa akiwa na AS Monaco analipwa Euro 350,000 kwa mwezi.
Alipokuwa Manchester United, alikuwa analipwa zaidi ya pauni 300,000 kwa wiki na hata baada ya kurejea Juventus, licha ya kupungua kwa mshahara wake, aliendelea kuwa mmoja wa wachezaji wanaolipwa vizuri zaidi nchini Italia.
Staa huyu pia ana mkataba na kampuni ya Adidas ambao alisaini nao kwa miaka 10 na kila mwaka inamlipa dola 4 milioni.
Mara kadhaa pia ameonekana katika matangazo ya kampuni ya Pepsi ambayo kwa mwaka inaripotiwa kumlipa dola 1 milioni.
Aliwahi kuwa na mikataba ya udhamini na kampuni kama TCL, Electronic Arts (EA Sports FIFA), na nyingine ndogondogo za mitindo na mavazi ambazo nyingi zilivunja mikataba baada ya kuona amefungiwa.
MAGARI YAKE
Rolls-Royce Wraith la dola 350,000
Ferrari 812 Superfast-dola 400,000
Mercedes GLS 4x4- dola 135,000
Lamborghini Aventador- dola 500,000
Bentley Continental GT - dola 220,000
Maserati Quattroporte - dola 140,000
NYUMBA
Pogba anamiliki nyumba ya kifahari nchini Uingereza ambayo alinunua wakati akiwa Manchester United. Nyumba hiyo ina chumba cha mazoezi, studio ya kurekodi muziki (kwa kuwa anapenda muziki), bustani kubwa, bwawa la kuogelea, na sehemu ya michezo ya watoto. Thamani ya mjengo huo inadaiwa kuwa ni pauni 2 milioni.
MSAADA KWA JAMII
Pogba amekuwa mstari wa mbele kusaidia jamii hasa kupitia taasisi yake ya Pogba Foundation inayojihusisha na kusaidia watoto na vijana hususani barani Afrika.
Aliwahi pia kusaidia wakimbizi kupitia mashirika ya misaada kama UNICEF na UNHCR, vilevile wakati wa janga la COVID-19 alichangia pesa kusaidia ununuzi wa vifaa vya kinga na amewahi kufadhili miradi ya maji safi na elimu katika nchi ya asili ya wazazi wake ya Guinea.
BATA NA MAISHA BINAFSI
Pogba yupo kwenye ndoa na mwanamitindo mzaliwa wa Bolivia, Maria Zulay Salaues, na wamebarikiwa watoto watatu, Pia ana ndugu zake wawili Mathias na Florentin Pogba ambao pia ni wachezaji.
Wakati amefungiwa kujihusisha na soka baadhi ya ripoti zilidai kuwa mke wake naye alimtenga lakini baadaye ikawekwa sawa kuwa Zulay hakuwahi kumwacha Pogba na muda wote ambao alikuwa anatumikia adhabu yeye ndio alisimama kama nguzo muhimu kwake.