Partey anyimwa viza kuingia Canada Kombe la Dunia
Muktasari:
- Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) limethibitisha kiungo huyo wa Villarreal amekataliwa kuingia Canada baada ya ombi lake la visa kukataliwa na mamlaka za nchi hiyo kutokana na kesi za ubakaji zinazomkabili nchini England.
WAKATI Ghana ikijiandaa kucheza mechi yake ya kwanza ya Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Panama Alhamisi ijayo mjini Toronto nchini Canada, itaikosa huduma ya kiungo wake, Thomas Partey.
Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) limethibitisha kiungo huyo wa Villarreal amekataliwa kuingia Canada baada ya ombi lake la visa kukataliwa na mamlaka za nchi hiyo kutokana na kesi za ubakaji zinazomkabili nchini England.
Kwa mujibu wa taarifa ya FIFA, Partey hataruhusiwa kusafiri kutoka kambi ya timu ya Ghana iliyopo Boston nchini Marekani, kuelekea Canada kwa ajili ya mchezo wao wa kwanza dhidi ya Panama utakaochezwa Juni 17, 2026.
“FIFA imethibitisha kwamba mchezaji Thomas Partey hataweza kusafiri kutoka kambi ya timu ya Ghana iliyopo Boston, Marekani, kwenda Canada kwa ajili ya mechi yao ya kwanza dhidi ya Panama Jumatano, Juni 17, kutokana na ombi lake la visa kukataliwa na serikali ya Canada,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.
FIFA pia imesisitiza kuwa haihusiki na taratibu za uhamiaji za nchi waandaaji wa mashindano, ikieleza kuwa mamlaka ya mwisho ya kutoa visa na kuruhusu wageni kuingia nchini hubaki mikononi mwa serikali husika.
Hata hivyo, Waziri wa Michezo wa Ghana, Kofi Adams, amesema hana taarifa zozote rasmi kwamba Partey amekataliwa visa ya kuingia Canada.
Akizungumza na vyombo vya habari, Adams amesema anafahamu kulikuwa na changamoto fulani za awali kuhusu visa ya Partey ya kuingia Marekani, lakini suala hilo lilitatuliwa na mchezaji huyo alipewa ruhusa ya kusafiri. Amesema hajapokea taarifa yoyote kutoka Shirikisho la Soka la Ghana (GFA) au viongozi wa timu kuhusu kukataliwa kwa visa ya Canada.
Licha ya kesi inayomkabili kuendelea, kocha wa Ghana, Carlos Queiroz, amemjumuisha Partey katika kikosi cha wachezaji 26 cha Kombe la Dunia, akisisitiza kuwa mchezaji huyo anapaswa kuchukuliwa kuwa hana hatia hadi mahakama itakapothibitisha vinginevyo. Ghana ipo Kundi L pamoja na Panama, England na Croatia ambapo mechi ya kwanza dhidi ya Panama itachezea nchini Canada, huku zingine mbili dhidi ya England na Croatia zikipigwa Marekani.
Partey alishtakiwa kwa mara ya kwanza mwaka 2025 kwa makosa matano ya ubakaji pamoja na kosa moja la unyanyasaji wa kingono.
Februari 2026, kiungo huyo aliongezewa mashtaka mengine mawili. Mashtaka hayo yanahusiana na matukio yanayodaiwa kutokea kati ya mwaka 2021 na 2022 alipokuwa akiichezea Arsenal.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 32, amekanusha mashtaka yote na amejibu mahakamani kuwa hana hatia. Kesi yake inatarajiwa kuanza kusikilizwa Novemba 2026, ingawa kuna uwezekano wa kuahirishwa hadi mwaka 2027.
Partey ni zao la akademi ya Atlético Madrid na alicheza mechi yake ya kwanza ya soka la kulipwa mwaka 2013. Baada ya kuitumikia Arsenal kwa misimu mitano, alijiunga na Villarreal CF kwa uhamisho wa bure Agosti 2025.
Msimu uliopita alicheza mechi 25 akiwa na Villarreal. Mkataba wake wa sasa unamalizika mwishoni mwa Juni 2026, lakini klabu hiyo ina chaguo la kumuongezea mkataba wa mwaka mmoja zaidi.
Katika ngazi ya timu ya taifa, Partey ameichezea Ghana mara 58 na alikuwa sehemu ya kikosi cha Black Stars kilichoshiriki Kombe la Dunia la mwaka 2022 nchini Qatar.