Kompyuta yaipa Arsenal ubingwa
Muktasari:
- Miamba hiyo ya Emirates imepewa asilimia 21.13 ya uwezekano wa kunyakua taji hilo, kwa mujibu wa utabiri wa kompyuta.
LONDON, ENGLAND: ARSENAL imepewa nafasi kubwa ya kushinda ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.
Miamba hiyo ya Emirates imepewa asilimia 21.13 ya uwezekano wa kunyakua taji hilo, kwa mujibu wa utabiri wa kompyuta.
Hii imekuja baada ya kuonyesha kiwango bora sana kwenye ushindi wao dhidi ya Atletico Madrid, ambao ulikuwa watatu katika mechi tatu za michuano hiyo ilizocheza msimu huu. Arsenal imezichapa pia Athletic Bilbao na Olympiakos na ndiyo maana kompyuta maalumu, inaamini ubingwa unaweza kunaswa na miamba hiyo inayonolewa na Mhispaniola, Mikel Arteta.
Kwenye utabiri wa timu zitakazofika fainali, kompyuta imetabiri Arsenal ina uwezekano wa asilimia 35.57. Na Washika Bunduki wana asilimia 54.38 ya uwezekano wa kufika nusu fainali ya michuano hiyo hasa baada ya kuanza kwa kiwango bora zaidi katika michuano hiyo.
Paris Saint-Germain, ambao ni mabingwa watetezi, nao wana asilimia 25.59 ya kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu, huku uwezekano wa kunyakua taji ukichuka, wakiwa na asilimia 14.03. Manchester City na Liverpool ni miongoni mwa timu zinazofukuzia ubingwa.
Man City ina asilimia 12.12 ya uwezekano wa kushinda ubingwa, wakati Liverpool ina asilimia 12.31 na hilo limekuja baada ya ushindi wao dhidi ya Eintracht Frankfurt.
Bayern Munich, Real Madrid na Inter Milan kwa mujibu wa utabiri wa kompyuta zina nafasi ndogo ya kunyakua ubingwa, lakini zipo kwenye kinyang'anyiro. Tottenham, ambayo ilishindwa kutamba mbele ya Monaco kwenye mchezo uliopita baada ya kutoka sare ya 0-0, ina asilimia 1.34 ya uwezekano wa kuwa bingwa na itakuwa mara yao ya kwanza endapo kama itashinda.
Chelsea iliyoshinda 5-1 kwenye mchezo uliopita dhidi ya Ajax ina asilimia 11.68 ya uwezekano wa kufika fainali, wakati kwenye orodha hiyo timu za chini Barcelona na Newcastle kwenye orodha ya timu zinazopewa nafasi ya kunyakua ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.