Nyota Arsenal azitamani fainali za Kombe la Dunia 2026
Muktasari:
- Martineli amekuwa akiitwa mara kadhaa kwenye kikosi cha taifa hilo linaloshikilia rekodi ya kutwaa Kombe la Dunia mara tano, ambapo mwaka 2022 alishiriki kwa mara ya kwanza fainali hizo nchini Qatar. Kwa sasa anatazamia fainali za mwakani zitakachezwa kwa mara ya 23, tangu kuanzishwa kwake mwaka 1930.
Nyota wa Arsenal, Gabriel Martinelli ameelezea shauku yake ya kutaka kuwa sehemu ya kikosi cha Brazil kitakachoshiriki fainali za Kombe la Dunia 2026, zitakazopigwa nchini Marekani, Mexico na Canada.
Martineli amekuwa akiitwa mara kadhaa kwenye kikosi cha taifa hilo linaloshikilia rekodi ya kutwaa Kombe la Dunia mara tano, ambapo mwaka 2022 alishiriki kwa mara ya kwanza fainali hizo nchini Qatar. Kwa sasa anatazamia fainali za mwakani zitakachezwa kwa mara ya 23, tangu kuanzishwa kwake mwaka 1930.
Martinelli mwenye umri wa miaka 24, amekuwa na kiwango bora akiwa na kikosi cha Arsenal, hali ambayo anaamini huenda ikamshawishi kocha mkuu wa Brazil, Carlo Ancelotti kumwita kwa ajili ya fainali za Kombe la Dunia, zilizopangwa kuanza Juni 11, 2026.
Amesema amekuwa na mwendelezo mzuri kwenye klabu yake, na sasa amejipanga kuisaidia nchi yake ili kufanikisha mpango wa kurejesha ubingwa wa dunia, ambao waliupoteza mwaka 2006, katika fainali zilizofanyika Ujerumani.
“Kombe la Dunia linakaribia, kila mtu anahamasika. Kwangu nina hamu ya kuwa sehemu ya kikosi cha taifa langu, ninaamini kwa mwendelezo wangu, kocha mkuu huenda akashawishika na kuniita kwenye kikosi chake.
“Japo ni mapema mno kuamini hilo, lakini nina shauku kubwa ya kutaka kucheza Fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza, nitafarijika mno ikitokea kocha Carlo ameniita kwenye kikosi chake, nitahakiksiha ninapambana na kuingia kwenye kikosi cha kwanza, ili niiwakilishe nchi yangu kwa vitendo,” amesema Martineli.
Akaongeza: “Ninalenga kushinda mataji na Arsenal na kuwa kwenye Kombe la Dunia. Nimekuwa nikifanya kazi kwa bidii, kikosi kizima kinataka kufika mbali na kushinda mataji. Tunajitolea zaidi na zaidi na kuzingatia maelezo madogo kutoka kwa kocha wetu.”
Martinelli ameshacheza mechi 11 msimu huu, tano kati ya hizo akiwa ameanza kwenye kikosi cha kwanza cha Arsenal. Kufuatia usajili mpya wa msimu huu wa klabu hiyo, kiungo huyo aliiweka hatarini nafasi yake kwenye kikosi cha kwanza cha Mikel Arteta, lakini amethibitisha bado ana uwezo wa kupambana na kuwa tegemeo kwa kocha huyo kutoka Hispania.
Katika Kombe la Dunia 2022, Martinelli alicheza mechi yake ya kwanza alipokuwa mchezaji wa akiba, akiingia uwanjani kuchukua nafasi ya Raphinha dakika ya 87, Brazil ikishinda 2–0 dhidi ya Serbia.
Martinelli hakutumika kwenye ushindi wa Brazil wa 1–0 dhidi ya Uswisi, lakini alicheza mechi yote wakati Brazil ilipofungwa 1–0 na Cameroon. Pia alihusika katika ushindi wa Brazil wa 4–1 dhidi ya Korea Kusini katika hatua ya 16 bora, akiingia kuchukua nafasi ya Vinícius Júnior dakika ya 72, na hakutumika kwenye mechi ya robo fainali dhidi ya Croatia, ambayo Brazil ilipoteza kwa mikwaju ya penalti 4–2 baada ya sare ya 1–1.
Novemba 16, 2023, Martinelli alifunga bao lake la kwanza kwa timu ya taifa ya Brazil katika kichapo cha 2–1 dhidi ya Colombia kwenye hatua ya kufuzu Kombe la Dunia la 2026. Pia Oktoba 2025, katika mechi ya kirafiki ambayo Brazil ilifungwa 3-2 na Japan, alifunga.
Ikiwa ataendelea na kiwango hicho, ana nafasi kubwa ya kuitwa na Carlo Ancelotti kwenye kikosi cha Kombe la Dunia mwakani. Ingawa bado miezi minane kabla ya kuanza kwa fainli hizo.