KOMBE LA DUNIA QATAR 2022: Vigezo kuitwa timu ya Taifa England

LONDON, ENGLAND.  MTOKO wa England kwenda Qatar kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 unazidi kuleta mzuka kwa mashabiki wake.

Kikosi chao cha Three Lions mechi yake ya kwanza kwenye Kundi B dhidi ya Iran imebakiza miezi miwili tu kufanyika kwenye fainali hizo, huko kocha wa mabingwa hao wa dunia wa mwaka 1966, Gareth Southgate akifanya maandalizi ya mwisho kabla ya kwenda kwenye mikikimikiki hiyo inayohesabika kama tamasha kubwa kabisa la mchezo wa soka duniani.

Mechi zijazo wa kimataifa ni nafasi nzuri na muhimu kwa kocha Southgate na benchi lake la ufundi kukamilisha mipango ya mwisho ya kupata wale wakati watakaopanda kwenye ndege yake kwa ajili ya kwenda kupiga mzigo huko Qatar 2022.

Je, ni wachezaji gani watachaguliwa na kuunda kikosi cha Gareth Southgate kwenye chama la England huko Qatar?

Kuteua kikosi cha wachezaji wa kwenda nao kwenye fainali za Kombe la Dunia siku zote umekuwa mjadala wa moto, hivyo suala la kuona kila mtu akitoa maoni yake ni mchezaji gani aende na nani abaki ni jambo litakalozungumzwa sana wakati fainali hizo zikiwa zinakaribia.

Kwa kikosi cha Three Lions, bila ya shaka, straika Harry Kane na kipa Jordan Pickford ni watu waliojihakikishia nafasi ya kuwamo kwenye timu labda tu kama watakuwa majeruhi. Lakini, nafasi nyingine za kujaza kwenye kikosi hicho bado zipo wazi na sasa ni suala la wachezaji wenyewe kupambana ndani ya miezi miwili iliyobaki ili kumshawishi kocha.

Mara nyingi makocha wanakwenda na wachezaji ambao wamekuwa wakifanya vizuri kwa mwaka husika wa fainali hizo, licha ya kwamba nao wamekuwa na machaguo yao kutokana na staili wanazokwenda kucheza kwenye mikikimikiki hiyo.

Lakini, kama Gareth Southgate ataamua kuteua kikosi chake kwa kulingana na wachezaji wenye thamani kubwa sokoni, kikosi chake kitakuwa na wakali ambao bila ya shaka watakwenda kuonyesha upinzani mkali kwenye mbio za kusaka ubingwa.

Kwa mujibu wa takwimu wa TransferMarkt, hii hapa orodha ya mastaa wa England wenye thamani kubwa sokoni, ambao kocha Southgate anaweza kuwateau na kupata kikosi cha kibabe kabisa kwa ajili ya fainali hizo za Qatar. Fomesheni ya kikosi 4-3-3.

Hiki hapa kikosi cha England kwenye Kombe la Dunia 2022 kama kitateuliwa kwa kuzingatia thamani za wachezaji wake sokoni.


Kipa: Jordan Pickford: Pauni 25.2 milioni

Pickford amekuwa akifanya vizuri sana anapokuwa na jezi za timu ya taifa ya England na bila ya shaka atakuwa chaguo la kwanza kwenye goli la timu hiyo wakati watakapokwenda kwenye mchakamchaka wa kusaka ubingwa wa dunia huko Qatar. Kipa huyo amekuwa mhimili mkubwa wa timu ya taifa ya England kwenye michuano ya kimataifa na atakuwa tumaini kubwa huko Qatar 2022.


Beki wa kushoto: Ben Chilwell: Pauni 34.2 milioni

Beki wa kati: Fikayo Tomori: Pauni 45 milioni

Beki wa kati: Ben White: Pauni 36 milioni

Beki wa kulia: Trent Alexander-Arnold: Pauni 72 milioni

Wakati ikitazamwa kama beki yenye mvuto wa kitazama na kuwa moto wanapokwenda mbele kushambulia, wasiwasi kwenye ukuta huu ni pale timu inaposhambuliwa na washambuliaji wakali kama Kylian Mbappe.

Itakuwa shughuli, lakini ni ukuta mzuri. Kwenye safu hii, pembeni England itaweza kushambulia muda wote, huko Ben White akiminika atakuwa kisiki imara kabisa katikati.


Kiungo wa kati: Phil Foden: Pauni 81 milioni

Kiungo wa kati: Jude Bellingham: Pauni 72 milioni

Kiungo mshambuliaji: Mason Mount: Pauni 67.5 milioni

Sehemu ya kiungo ndiyo itakayokuwa mjadala mkubwa katika kuelekea kwa fainali hizo za Qatar.

Wakali hao wote watatu watakaokuwa katikati ya uwanja wote wana vipaji vikubwa vya soka, lakini wakicheza pamoja kikosi kitakuwa na udhaifu katikati. Silaha kubwa ya safu hiyo ya kiungo ni kuwafanya kuwa na mpira muda wote, watumie staili hiyo ya kukama kwa kumiliki mpira.


Winga wa kushoto: Jadon Sancho: Pauni 67.5 milioni

Winga wa kulia: Bukayo Saka: Pauni 63 milioni

Mshambuliaji wa kati: Harry Kane: Pauni 81 milioni

Ni safu nyingine matata kabisa kwenye kikosi cha England, lakini kwa kocha Southgate haliwezi kuwa chaguo lake. Kane, hakuna ubishi ataongoza safu ya ushambuliaji, shida itakuwa kwa hao wawili waliobaki.

Lakini, kama atawachagua, hawatamwangusha, hakika mabeki wa timu pinzani watakuwa kwenye wakati mgumu muda wote kutokana na kasi ya fowadi hiyo.