KOMBE LA DUNIA QATAR 2022: Al Rihla, gozi lililojaa teknolojia

DOHA, QATAR. AL Rihla. Ndo jina la mpira utakaotumika kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 huko Qatar. Maana ya Al Rihla ni safari. Hivyo, safari inaanzia Qatar.

Mastaa wa soka kama Harry Kane, Cristiano Ronaldo, Lionel Messi, Kylian Mbappe, Robert Lewandowski, Neymar - Al Rihla itakuwa kwenye miguu yao, watakapojaribu kumsaka bingwa wa dunia kwenye mchakamchaka wa fainali hizo zitakazofanyika mwisho wa mwaka kwa mara ya kwanza kwenye historia yake. Kombe la Dunia 2022 huko Qatar litaanza Novemba 20 hadi Desemba 18.

Hii ni mara ya 14 mfululizo mpira wa Kombe la Dunia ukitengenezwa na Adidas, kampuni ya Kijerumani, ambayo imepewa dhamana hiyo kutengeneza mpira wa michuano mikubwa.

Al Al Rihla umetengenezwa kwa dizaini za kibabe kabisa na teknolojia ya hali ya juu, ambapo kwa nje unaonekana kuwa na boti, bendera ya Qatar, maumbo ya pembetatu yaliyotengenezwa kuzunguka duara hilo la mpira. Sambamba na hilo kuna nembo halisi ya fainali za Kombe la Dunia huko Qatar na logo ya Adidas, ambayo ni ile mistari mitatu.


AL RIHLA UKOJE?

Ukifahamika kama mpira rasmi kwa fainali za Kombe la Dunia 2022 huko Qatar, Al Rihla unatajwa kuwa mpira uliotengenezwa kwa teknolojia ya kiwango cha juu. Mpira huo una uwezo wa kutembea kwa kasi kubwa hewani kuliko mipira mingine yote iliyowahi kutumika kwenye fainali za Kombe la Dunia. Makipa watakaoenda na timu zao huko Qatar watakuwa kwenye kasheshe kwelikweli kuwakabili mastaa wanaopiga mashuti kama Luka Modric.

“Soka imekuwa kasi sana, mbio hivyo usahihi wa mpira unapokuwa hewani ni kitu muhimu. Dizaini mpya ya mpira unaruhusu kuwa na kasi na kusafiri kwa nguvu ileile unapokuwa hewani,” alisema Franziska Loeffelmann, mkurugenzi wa dizaini wa Adidas.

“Hii ni steji kubwa kabisa katika michezo yote, tumefanya kusichowezekana kuwezekana kwa kutengeneza mpira utakaokuwa na kasi zaidi kwenye Kombe la Dunia.”


AL RIHLA NI TEKNOLOJIA TUPU

Kutokana na mtazamo wa kutaka kuwasaidia waamuzi kwenye Kombe la 2022, adidas iliamua kuufanya mpira wa Al Rihla kuwa wa kiteknolojia zaidi ili kuwarahisishia waamuzi watakaokuwa kwenye VAR na kusaidia maamuzi ya wachezaji kuotea. Teknolojia hiyo imewekwa ndani ya mpira, ambapo taarifa za mapema zitakuwa zimetumwa kwa mwamuzi ili kufanya uamuzi wa mapema linapokuja suala la mabao yanayofungwa kama mfungaji aliotea au la ili kuepuka masuala ya kupoteza muda. Kikubwa mpira utakuwa unasaidia ishu ya offside na VAR. Ulifanyika utafiti wa miaka mitatu hadi kuja na teknolojia hiyo matata kabisa ya kuweka ndani ya mpira ambao utatumika kwenye steji kubwa ya soka duniani. Ndani ya mpira huo kuna sensa na betri la kuchaji, ambapo litakuwa likichajiwa bila ya waya.


AL RIHLA UNAUZWA WAPI?

Al Rihla upo tayari unapatikana kwenye maduka ya mtandao ya Adidas.com. Mpira rasmi ambao utatumika kwenye Kombe la Dunia huko Qatar bei yake ni Pauni 130, wakati ule utakuwa unaofanana ambao si wenyewe, utapatikana kwa Pauni 30.