Kofane kufuata nyayo za Roger Milla, Eto’o
Muktasari:
- Kwa kuitikia wito wa taifa lake katika AFCON, Kofane amejiunga na orodha ya washambuliaji wakubwa waliowahi kuitumikia Cameroon, akifuata nyayo za mastaa kama Roger Milla na Samuel Eto’o.
CASABLANCA, MOROCCO: MSHAMBULIAJI kijana wa Cameroon, Christian Michel Kofane ameandika historia mapya katika Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), baada ya kung’ara akiwa na umri wa miaka 19 tu.
Kwa kuitikia wito wa taifa lake katika AFCON, Kofane amejiunga na orodha ya washambuliaji wakubwa waliowahi kuitumikia Cameroon, akifuata nyayo za mastaa kama Roger Milla na Samuel Eto’o.
Licha ya umri mdogo, ameonyesha ukomavu mkubwa uwanjani na uwezo wa kubeba presha katika mechi muhimu.
Akikumbuka safari yake, Kofane amesema, “Nilianza AS Vatican kabla ya kuhamia AS Nylon ambako mpira wa tiki-taka unahimizwa. Huo ndio ulikuwa msingi wangu, ndiyo maana nilipofika Ulaya niliweza kuzoea haraka, ingawa haikuwa rahisi.”
Historia ya Cameroon katika mashindano ya AFCON imejengwa na washambuliaji waliokuwa na kipaji. Roger Milla aliiongoza timu hiyo kutwaa ubingwa mwaka 1988, huku Samuel Eto’o akivunja rekodi nyingi na kuwa mfungaji bora wa muda wote wa AFCON. Sasa, Kofane anaona fahari kuonyesha makali yake.
Ubora wake ulianza kujidhihirisha alipokuwa mfungaji bora katika mashindano mbalimbali ya vijana nchini Cameroon, hali iliyomfungulia mlango wa kwenda barani Ulaya na kujiunga na Albacete ya Hispania.
Majira ya joto yaliyopita, Kofane alipiga hatua nyingine kubwa kwa kujiunga na Bayer Leverkusen ya Ujerumani, ambako aliweka rekodi kwa kuwa mfungaji mdogo zaidi wa klabu hiyo katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Akizungumzia tukio hilo, amesema, “Nilipokutana na Samuel Eto’o baada ya mechi ya Ligi ya Mabingwa, alinipa ushauri mkubwa. Aliniambia niwe nafanya maamuzi haraka katika mechi kubwa, kwa sababu huko ndiko wachezaji wakubwa hutambulika.”
Katika AFCON, Kofane alionyesha kiwango kizuri katika mechi ya robo fainali dhidi ya Msumbiji, alifunga bao la ushindi, akachaguliwa Mchezaji Bora wa Mechi na kuisaidia Cameroon kupata ushindi muhimu.