Kocha wa Jamhuri ya Ireland afichua alichoambiwa na Ronaldo
Muktasari:
- Ronaldo alionyeshwa kadi nyekundu, wakati Jamhuri ya Ireland ikiichapa Ureno 2–0 katika jana Alhamisi, Novemba 13, kwenye Uwanja wa Aviva mjini Dublin, Ireland.
Kocha wa Jamhuri ya Ireland, Heimir Hallgrímsson, amefichua kile ambacho Cristiano Ronaldo alimwambia baada ya nyota huyo wa Ureno kupewa kadi nyekundu wakati wa mechi ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 iliochezwa jana Alhamisi, Novemba 13.
Ronaldo alionyeshwa kadi nyekundu, wakati Jamhuri ya Ireland ikiichapa Ureno 2–0 katika jana Alhamisi, Novemba 13, kwenye Uwanja wa Aviva mjini Dublin, Ireland.
Awali, Ronaldo alipewa kadi ya njano, lakini mwamuzi Glenn Nyberg alitakiwa na VAR kupitia tukio hilo, ndipo alipojiridhisha na kubadilisha adhabu na kumuonyesha kadi nyekundu ya moja kwa moja.
Hallgrímsson, amesema baada ya tukio hilo, Ronaldo alimpa pongezi kwa kumtengenezea mbinu zilizomsababishia adhabu ya kadi nyekundu inayomnyima nafasi ya kuwa sehemu ya kikosi cha Ureno, katika mechi ya mwisho wa kufuzu Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Armenia, utakaopigwa wiki ijayo.
“Alinisifu kwa kumwekea mtego uliosababishwa na mbinu zangu ambazo zilipelekea kumpa presha, lakini mimi sikuhusika katika tukio ambalo amelifanya akiwa uwanjani, kilichomsababishia kadi nyekundu ni kitendo chake mwenyewe,” Hallgrímsson amesema na kuongeza;
“Mimi sikufanya kitu chochote, zaidi ya kutumia mbinu zangu kama kocha ili tushinde mechi iliyokuwa inatukabili na kweli tumeshinda, lakini nimemuelewa kwa maneno yake aliyoniambia, kwani yanatokana na fikra zake mwenyewe.”
“Aliniambia kuwa ulikuwa ni mtego maalum niliomwekea kijanja, pia alimlaumu mwamuzi kwa adhabu aliyompa, japo ninaamini anaendelea kujutia tukio hilo litakalomnyima nafasi ya kucheza mechi inayofuata," ameongeza kocha huyo.
Mabao mawili ya Troy Parrott yaliipa Ireland ushindi wa 2–0 dhidi ya Ureno kwenye Uwanja wa Aviva mjini Dublin, na kuweka hai matumaini ya taifa hilo kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026.
Matumaini ya Ureno ya kupata sare au ushindi yafifia baada ya Ronaldo kuonyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya 62.
Mshambuliaji huyo wa Al-Nassr, alimpiga bega kwa kiwiko beki wa Ireland Dara O’Shea baada ya wawili hao kushindana kuwania mpira.