Kisa kadi nyekundu, Martinez amkingia kifua Ronaldo
Muktasari:
- Ronaldo alionyeshwa kadi hiyo wakati Jamhuri ya Ireland ikichapa Ureno 2–0 jana Alhamisi, Novemba 13 kwenye Uwanja wa Aviva mjini Dublin, Ireland.
Kocha wa timu ya taifa ya Ureno, Roberto Martínez, amemkingia kifua nahodha na mshambuliaji wa kikosi hicho, Cristiano Ronaldo, kufuatia adhabu ya kadi nyekundu aliyopewa katika mechi ya kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Jamhuri ya Ireland.
Ronaldo alionyeshwa kadi hiyo wakati Jamhuri ya Ireland ikichapa Ureno 2–0 jana Alhamisi, Novemba 13 kwenye Uwanja wa Aviva mjini Dublin, Ireland.
Akizungumza kuhusu tukio hilo, Martínez amejaribu kumtetea Ronaldo, akisisitiza mchezaji huyo wa klabu ya Al-Nassr inayoshiriki Ligi Kuu Saudi Arabia, alijaribu kumsukuma O’Shea kwa sababu mabeki walikuwa wakimsumbua kwa kumvuta.
“Ni vigumu kwa mchezaji kama Cristiano kuwa katika eneo la hatari na kilichotokea ni hatua ya kujihani kutokana na kadhia aliyokuwa akiipata kutoka kwa wachezaji wa timu pinzani,” Martínez amesema.
“Alipata wakati mgumu sana kila apokuwa kwenye jukumu lake la ushambulizi kwenye lango la wapinzani wetu na hilo lilitokea mara kwa mara. Ukiangalia kwa umakini utagundua hakukuwa na vurugu, bali alijaribu tu kuwasukuma waondoke.
“Ronaldo alikuwa na bahati mbaya. Nafikiri picha video inafanya ionekane kuwa ni tukio baya kuliko uhalisia ulivyokuwa. Hii ndio kadi yake ya kwanza nyekundu akiwa na timu ya taifa, ni jambo la ajabu sana," ameongeza Martinez.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 40 alimpiga bega kwa mkono beki Dara O’Shea baada ya wawili hao kushindana kuwania mpira.
Awali, Ronaldo alipewa kadi ya njano, lakini mwamuzi Glenn Nyberg alitakiwa na VAR kupitia tukio hilo, ndipo alipojiridhisha na kubadilisha adhabu na kumuonyesha kadi nyekundu ya moja kwa moja.
Kwa mantiki hiyo Ronaldo atakosa mechi mbili zinazoratibiwa na FIFA, ambapo mechi ya kwanza itakuwa ya mwisho ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Armenia, kisha ataendelea na adhabu kwenye mechi ya kwanza ya fainali za Kombe la Dunia 2026, endapo Ureno itafuzu.