Kocha Spurs lolote linaweza kutokea
Muktasari:
- Aliyewahi kuwa kipenzi cha mashabiki wa Spurs, Mauricio Pochettino ni miongoni mwa makocha wanaotajwa kuchukua nafasi hiyo moja kwa moja baada ya Kombe la Dunia 2026, atakapomaliza majukumu yake na timu ya taifa ya Marekani,
LONDON, ENGLAND: TOTTENHAM inaangalia kocha mbadala atakayekuja kurithi mikoba ya Thomas Frank ambaye yupo kwenye hatari kubwa ya kufutwa kazi.
Aliyewahi kuwa kipenzi cha mashabiki wa Spurs, Mauricio Pochettino ni miongoni mwa makocha wanaotajwa kuchukua nafasi hiyo moja kwa moja baada ya Kombe la Dunia 2026, atakapomaliza majukumu yake na timu ya taifa ya Marekani, huku jina jingine linalotajwa ni Xavi, ambaye kwa sasa hana klabu, gwiji wa Nou Camp aliyewaongoza Barcelona kutwaa ubingwa wa La Liga mwaka 2023.
Viongozi wa klabu wanapima uwezekano wa kumtimua kabla ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa, Jumanne dhidi ya Borussia Dortmund, katika mabadiliko makubwa ya msimamo wao wa awali na endapo ataondoka kabla ya mchezo huo, kocha msaidizi aliyeteuliwa hivi karibuni, John Heitinga, anaweza kuwa chaguo la kwanza la kocha wa mpito.
Cha kushangaza, Frank ndiye aliyesukuma zaidi usajili wa Heitinga, ambaye pia aliwahi kufanya kazi chini ya Arne Slot huko Liverpool walipotwaa ubingwa wa Ligi Kuu England msimu uliopita.
Haya yanajiri baada ya uongozi, ambao awali ulikuwa thabiti kumuunga mkono kocha huyo raia wa Denmark, kutambua ukubwa wa hasira za mashabiki baada ya kipigo cha mabao 2-1 nyumbani dhidi ya West Ham, timu inayopambana kuepuka kushuka daraja.
Kipigo hicho kimeiacha Spurs ikisota nafasi ya 14 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, ikiwa pointi nane nyuma ya tano bora na pointi 10 juu ya eneo la kushuka daraja.
Hata hivyo, inaelezwa viongozi wakuu pia wanataka kusikia maoni ya wachezaji ili kutathmini kama bado kuna uungwaji mkono wa ndani kwa kocha huyo wa zamani wa Brentford.
Hata hivyo, kuna hisia zinazoongezeka, Frank ameshindwa kurejesha mamlaka ndani ya kikosi na suluhisho bora kwa pande zote linaweza kuwa kumaliza haraka utawala wake wa miezi saba uliogubikwa na matatizo.
Frank aliendesha mazoezi na kikao cha kurejesha nguvu Jumapili kama kawaida, huku wachezaji wakibaki gizani kuhusu mustakabali wa kocha wao na alisimamia mazoezi ya Jumatatu kwa ajili ya mchezo dhidi ya Dortmund.