Kocha afichua Benfica ilivyomkosa Joao Felix
Muktasari:
- Katika mahojiano na A Bola, Bruno Lage amesema Benfica walijitahidi kwa kila njia kumsajili Felix lakini walishindwa kufikia masharti ya Chelsea.
ALIYEKUWA kocha wa Benfica, Bruno Lage, amefichua sababu za klabu hiyo kushindwa kumsajili Joao Felix kutoka Chelsea wakati wa msimu wa joto, na hatimaye akatimkia Al-Nassr ya Saudi Arabia.
Katika mahojiano na A Bola, Bruno Lage amesema Benfica walijitahidi kwa kila njia kumsajili Felix lakini walishindwa kufikia masharti ya Chelsea.
Amesema Chelsea walikuwa na nia ya kulinda uwekezaji wao mkubwa kwa mchezaji huyo na walitaka kurejesha kiasi kikubwa cha fedha walicholipa awali.
"Nilianza kuamini Joao angeweza kuja. Lakini kwa kipindi hicho nilikuwa likizo. Nilikuwa uwanja wa ndege nilipopokea taarifa yake na nikampigia simu. Nilizungumza naye nikamwambia mambo mengi kuhusu klabu yetu, alitamani kuja kujiunga nasi tena, nilimuahidi ningezungumza na rais kutimiza matakwa yake, lakini bado ilishindikana.
"Chelsea ambayo ililipa kiasi kikubwa kwa Joao, haikuwa tayari kupunguza masharti ya malipo, na ilikuwa vigumu sana kwa Benfica, licha ya kufanya kila liwezekanalo kumrudisha nyumbani. Joao alionyesha hamu kubwa ya kurejea Benfica na pia alielewa kikamilifu timu niliyokuwa nikijaribu kuijenga, ambapo angekuwa sehemu muhimu sana, lakini mahitaji ya Chelsea yalikuwa hayatekelezeki," amesema Lage.
Joao Felix hatimaye alijiunga na klabu ya Al-Nassr ya Saudi Arabia, ambako sasa anacheza pamoja na Cristiano Ronaldo.
Chelsea walikubali dili ambalo linaweza kufikia Euro 50 milioni kwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25, ambaye amekuwa akisajiliwa na klabu kadhaa katika miaka ya hivi karibuni.
Joao alianza soka la ushindi akiwa na kikosi cha Benfica B mwaka 2016 hadi 2018, kabla ya kupandishwa kwenye kikosi cha wakubwa 2018–2019. Aliitumikia Atlético Madrid 2019 hadi 2024, ambapo mwaka 2023 alitua Chelsea kwa mkopo.
Msimu wa 2023–2024, alisajiliwa kwa mkopo Barcelona na msimu uliofuata alirudi Chelsea kwa kusajiliwa moja kwa moja kabla ya kuuzwa Al Nassr wakati wa majira ya kiangazi.