Kobbie Mainoo amuumbua Ruben Amorim
Muktasari:
- Kocha wa muda, Michael Carrick sasa ameshinda mechi tatu mfululizo tangu achukue mikoba Man United, jambo lililomchukua Amorim mwaka mzima kulifikia. Carrick pia amesimamia ushindi dhidi ya Manchester City, Arsenal na sasa Fulham akitegemea kiungo thabiti cha Mainoo na Casemiro, muunganiko ambao Amorim alikuwa akisita kuutumia.
MANCHESTER, ENGLAND: RUBEN Amorim aliamini Kobbie Mainoo hangeweza kucheza sambamba na Casemiro akiona hana nguvu, kasi wala uzoefu.
Lakini, mchezaji huyo aliyekulia akademi ya Manchester United ameacha nyuma miezi 14 migumu chini ya Amorim baada ya kuonyesha kiwango cha juu tena katika ushindi wa kusisimua wa Mashetani Wekundu wa mabao 3-2 dhidi ya Fulham uwanjani Old Trafford, Jumapili.
Kocha wa muda, Michael Carrick sasa ameshinda mechi tatu mfululizo tangu achukue mikoba Man United, jambo lililomchukua Amorim mwaka mzima kulifikia. Carrick pia amesimamia ushindi dhidi ya Manchester City, Arsenal na sasa Fulham akitegemea kiungo thabiti cha Mainoo na Casemiro, muunganiko ambao Amorim alikuwa akisita kuutumia.
Mainoo alipata nafasi yake ya nne mfululizo ya kuanza katika mashindano yote baada ya Carrick na kocha wa muda Darren Fletcher kuachana na mfumo wa Amorim wa 3-4-2-1. Wakati Man United ilipata shida ikiwa na viungo wawili katikati chini ya Amorim na huenda ingekuwa hivyo pia dhidi ya Fulham kama mfumo huo ungetumika, lakini sasa Mainoo na Casemiro walionekana imara sana katika mfumo wa 4-2-3-1.
Baada ya ushindi wa kusisimua uliopatikana dakika za majeruhi dhidi ya Fulham, Carrick alimpongeza Mainoo akisema ni “furaha kumtazama”.
Timu ya Marco Silva ilitishia sana kupitia katikati ya uwanja katika Old Trafford, na Casemiro pamoja na Mainoo walikuwa na kazi kubwa ya kufanya.
Kiungo nguli wa zamani Carrick, 44, amesema: “Kwa kweli Kobbie alikuwa mzuri sana leo kwa namna nyingi tena.
“Unaweza kuona namna Fulham wanavyocheza na kuzidisha idadi katikati ya uwanja, kulikuwa na kazi nyingi kwa Kobbie na Cassie kufanya, hasa eneo la kati.
“Hiyo ilikuwa bila mpira, na nilidhani alikuwa bora sana. Halafu akiwa na mpira, nimesema mara kadhaa, ana uwezo wa kustahimili presha, hashtuki kabisa.
“Anacheza mchezo wake tu. Anaelewa kinachohitajika na huchagua nyakati sahihi za kuonyesha ubora wake.
“Hivi ndivyo tunavyoanza kumzoea, na ninavyoanza kumzoea pia, lakini unasahau bado ni mchezaji mchanga sana.
“Ana mengi bado ya kuja, lakini kumuona leo akicheza kwa kujiamini na imani kubwa, ni furaha kubwa kumtazama, kwa kweli, kwa mchezaji kijana yeyote.”