Kisa Uefa Benjamin Sesko anukia Arsenal, Chelsea

Muktasari:
- Moja kati ya mambo ambayo Sesko amewaambia mabosi wa Leipzig ni ataondoka msimu ujao ikiwa timu hiyo haitofuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.
CHELSEA na Arsenal zinataka kutumia hali mbaya ya matokeo ya RB Leipzig kwa ajili ya kuhakikisha inaipata saini ya mshambuliaji wa timu hiyo na Slovenia, Benjamin Sesko dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Tangu kuanza kwa msimu huu Leipzig haipo katika kiwango bora na hadi sasa inashika nafasi ya sita katika msimamo wa Bundesliga hali inayowaweka katika nafasi mbaya kwenye kufuzu Ligi ya Mabingwa msimu ujao.
Moja kati ya mambo ambayo Sesko amewaambia mabosi wa Leipzig ni ataondoka msimu ujao ikiwa timu hiyo haitofuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Ikiwa itashindwa kufuzu kucheza michuano hiyo, Leipzig pia itahitajika kuuza baadhi ya wachezaji ili kuendana na sheria za matumizi ya pesa.
MANCHESTER City na Manchester United zinapambana vikali kwa ajili ya kuipata saini ya winga wa Sporting Lisbon na timu ya taifa ya Ureno, Francisco Trincao, 25, dirisha hili. Trincao ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwakani. Tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 40 za michuano yote na kufunga mabao tisa na kutoa asisti 13.
MANCHESTER United inataka kupambana na Arsenal ili kuipata huduma ya kiungo wa Real Sociedad na Hispania Martin Zubimendi, 26, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Zubimendi ambaye amekuwa akihusishwa na timu mbalimbali barani Ulaya kutokana na kiwango bora alichoonyesha akiwa na Sociedad, mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.
EVERTON itakumbana na upinzani mkubwa kutoka kwa Newcastle na Nottingham Forest katika mpango wao wa kutaka kumsajil winga wa Marseille, Luis Henrique, 23, dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Enrique ambaye msimu huu amecheza mechi 26 za michuano yote na kufunga mabao tisa, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.
TOTTENHAM imeingia kwenye vita dhidi ya Brighton na baadhi ya timu nyingine barani Ulaya kwa ajili ya kumsajili beki wa kulia wa Rayo Vallecano na Romania, Andrei Ratiu, 26, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Ratiu ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2028. Msimu huu amecheza mechi 25 za michuano yote.
TOTTENHAM imeendelea kushikilia msmamo wake wa kutomsainisha mkataba wa kudumu mshambulaiji wao raia wa Ujerumani, Timo Werner, 28, dirisha lijalo la majira ya kiangazi licha ya kuwepo kwa kipengele. Katika mkataba wake wa mkopo wa kuichezea Spurs, kuna kipengele ambacho kinaiwezesha kumnunua mazima kwa Pauni 8.5 milioni ikiwa atahitaji kufanya hivyo.
NEWCASTLE ipo tayari kukubali ofa itakayoanzia Pauni 10 milioni hadi Pauni 15 milioni ili kumuuza kipa wao raia wa England, Nick Pope, 32, dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Vigogo hao wanataka kumuuza ili kupata pesa itakazotumia kukamilisha dili la kumsajili nyanda wa Burnley na England, James Trafford, 22.
BARCELONA ipo kwenye mazungumzo ya kumuongeza mkataba mpya winga wao raia wa Brazil Raphinha, 28, ili kuendelea kuwa naye kwa muda mrefu zaidi. Raphinha ambaye kwa sasa ni mmoja wa mastaa tegemeo kikosi cha kwanza cha Barca, msimu huu amecheza mechi 39 za michuano yote na kufunga mabao 24, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.