Kisa mwamuzi, kocha Chelsea achefukwa
Muktasari:
- Newcastle iliibuka na ushindi katika uwanja wa Stamford Bridge kwa mara ya kwanza katika miaka 14 baada ya bao la dakika ya 18 la Anthony Gordon kuadhibu makosa ya ulinzi ya Chelsea na kufanya mechi hiyo kumalizika kwa ushindi wa 1–0.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Chelsea, Liam Rosenior amemlaumu mwamuzi Paul Tierney kutokana na kitendo cha ajabu alichoonyesha cha kuingilia majadiliano ya wachezaji wake kabla ya mechi dhidi ya Newcastle United.
Newcastle iliibuka na ushindi katika uwanja wa Stamford Bridge kwa mara ya kwanza katika miaka 14 baada ya bao la dakika ya 18 la Anthony Gordon kuadhibu makosa ya ulinzi ya Chelsea na kufanya mechi hiyo kumalizika kwa ushindi wa 1–0.
Tierney alionekana akitabasamu baada ya kukumbatiana na Cole Palmer katika mduara ambao nyota wa Chelsea walikuwa wakijadili mambo yao kabla ya mchezo huo uliomalizika kwa kukubali kichapo cha bao 1-0 ugenini.
Hata hivyo, baada ya mchezo kumalizika, mjadala mkubwa ulikuwa juu ya tukio hilo la ajabu na mwamuzi Tierney alisimama katikati ya duara la wachezaji wa Chelsea wakati nahodha wa timu hiyo, Reece James alipokuwa akizungumza na wachezaji wenzake.
Kocha Rosenior alisema atawasiliana na Professional Game Match Officials Limited (PGMOL), chombo kinachosimamia waamuzi wa mechi, ili kupata ufafanuzi kuhusu sababu ya kuvurugwa kwa utaratibu wa kawaida wa wachezaji wa Chelsea kabla ya mchezo huo.
Rosenior aliongeza, hakuzungumza na Tierney siku hiyo kwa sababu aliona si wakati sahihi kufanya hivyo.
“Sikuzungumza na Paul leo, sikuona kama ni jambo sahihi kufanya. Lakini nitawasiliana na Professional Game Match Officials Limited (PGMOL). Nitazungumza na waamuzi ili kuelewa vizuri nini hasa kilitokea.”
Katika mechi hiyo, inadaiwa Newcastle ilipaswa kuanza mchezo na mpira ulikuwa tayari karibu na eneo la katikati ya uwanja, huku Tierney akiwa amesimama karibu nao na kuonekana kama hataki kuondoka wakati wachezaji wa Chelsea walipokusanyika karibu na mpira huo.
Rosenior alidai pia mwamuzi huyo alipaswa kutoa penalti kwa tukio la Nick Woltemade kumsukuma Palmer.
Alisema kama mwamuzi Tierney angezingatia zaidi kazi yake ya kufanya maamuzi sahihi, basi timu yake ingepewa penalti katika mchezo huo.
“Kama Paul angejikita zaidi kwenye kazi yake, ambayo ni kufanya uamuzi sahihi, leo tungepewa penalti,” alisema.
“Siamini kama kuna mtu yeyote anaweza kusema Nick Woltemade hakumchezea vibaya Cole Palmer ndani ya eneo la hatari.”
Kwa upande wake, kocha wa Newcastle, Eddie Howe alipoulizwa kuhusu tukio hilo, alisema: “Hiyo haina umuhimu kwangu. Sijihusishi na mambo kama hayo; hayatatusaidii kushinda au kupoteza mchezo.”