Kisa Man United, FA yaipiga faini Chelsea
Muktasari:
- Kwa mujibu wa Daily Mail, hali hiyo imesababisha Chelsea kupigwa faini ya pauni 25,000 (Sh82.9 milioni za Kitanzania), kwani FA hutoa adhabu ya kifedha kwa timu inayopata kadi zisizopungua sita katika mechi moja.
KLABU ya Chelsea imepigwa faini na Shirikisho la Soka England (FA) baada ya kupata idadi kubwa ya kadi katika mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya Manchester United uliochezwa wikiendi iliyopita.
Kwa mujibu wa Daily Mail, hali hiyo imesababisha Chelsea kupigwa faini ya pauni 25,000 (Sh82.9 milioni za Kitanzania), kwani FA hutoa adhabu ya kifedha kwa timu inayopata kadi zisizopungua sita katika mechi moja.
Chelsea inaifahamu vyema adhabu hii, kwani msimu uliopita ilipigwa faini mara tatu kwa kosa hilo hilo. Ilianza kwa faini ya pauni 25,000 baada ya kupata kadi nane dhidi ya Bournemouth, Septemba 2024, kisha faini ikapanda hadi pauni 50,000 (Sh165.8 milioni za Kitanzania) kwa kadi sita dhidi ya Nottingham Forest, Oktoba 2024, na baadaye kufikia pauni 75,000 (Sh248.7 milioni za Kitanzania) baada ya kadi sita zaidi dhidi ya Newcastle mwezi huohuo.
Mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Old Trafford Jumamosi iliyopita, ulimalizika kwa wenyeji Manchester United kushinda mabao 2-1.
Katika dakika ya tano ya mechi hiyo, kipa wa Chelsea, Robert Sánchez, alionyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja.
Mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha Manchester iliongeza hali ya vurugu, huku Manchester United pia ikipoteza mchezaji wao Casemiro kwa kadi nyekundu baada ya kuonyeshwa kadi ya pili za njano kabla ya mapumziko.
Hata hivyo, Chelsea ndio iliyokuwa na makosa mengi ya kinidhamu, ikipokea jumla ya kadi sita zikiwemo tano za njano kwa wachezaji wake Marc Cucurella, Trevoh Chalobah, Enzo Fernández, Tosin Adarabioyo na Tyrique George, sambamba na kadi nyekundu ya kipa wao.
Klabu hiyo inaonekana kuwa na tatizo la nidhamu, kwani tayari imekusanya kadi 12 za njano na moja nyekundu katika mechi tano za Premier msimu huu. Timu nne pekee ndizo zilizopokea kadi nyingi zaidi (Bournemouth – 14, Crystal Palace – 13, Everton – 13 na Brighton – 13), lakini hakuna kati yao iliyopokea kadi nyekundu.
Takwimu zinaonyesha Chelsea ndiyo klabu iliyopokea kadi nyingi zaidi katika misimu miwili iliyopita.
Msimu uliopita, baada ya wachezaji wake kuendelea kupata kadi nyingi, kocha Enzo Maresca aliulizwa kama kikosi chake kina tatizo la nidhamu, lakini akapunguza uzito wa suala hilo.
Alisema: “Ni kitu cha kuboresha, lakini kwa ujumla ninapenda jinsi timu inavyopigana. Ninapenda jinsi wanavyokuwa kitu kimoja katika mapambano haya. Sioni kama kuna tatizo kubwa. Bila shaka kuna mambo tunaweza kuyadhibiti na kuyafanya vizuri zaidi, na hili ni moja ya mambo hayo. Lakini nikizungumzia roho ya timu na mshikamano wao, nimeridhika kabisa.”
Kuhusu faini, kocha huyo alitania kwa kusema: “Mimi siyo nitakayelipa!”
Chelsea inarejea tena uwanjani Jumamosi hii kwenye Ligi Kuu England ikiikaribisha Brighton. Pamoja na idadi kubwa ya kadi ilizopata wiki iliyopita, itaingia kwenye mechi hiyo ikiwa na wachezaji wake wote.
Kipa Robert Sánchez, aliyesimamishwa kutokana na kadi nyekundu dhidi ya Manchester United, alimaliza adhabu yake kwenye mchezo wa Kombe la Carabao dhidi ya Lincoln City katikati ya wiki, na yupo tayari kurejea uwanjani dhidi ya Brighton.