Kisa Liverpool, Gerrard amvaa Arne Slot
Muktasari:
- Baada ya kushinda mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Marseille kwa mabao 3-0, Slot alisema timu yake huwa inapata tabu inapokutana na mpinzani anayepaki basi na hiyo huchangia wao kupata matokeo mabovu.
LIVERPOOL, ENGLAND: LEJENDI wa Liverpool, Steven Gerrard amemwonya kocha wa timu hiyo, Arne Slot aache kulalamikia na kusema udhaifu wa Liverpool kwenye mahojiano na badala yake atafute suluhisho.
Baada ya kushinda mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Marseille kwa mabao 3-0, Slot alisema timu yake huwa inapata tabu inapokutana na mpinzani anayepaki basi na hiyo huchangia wao kupata matokeo mabovu.
Kocha huyo raia wa Uholanzi, alinukulia mara kwa mara msimu huu akielezea tatizo hilo na juzi baada ya mechi dhidi ya Marseille licha ya ushindi alirudia tena kusema.
"Ninajua vizuri kabisa kwa nini hatupati matokeo mazuri. Huwa tunapata urahisi pale mchezo unapokuwa wazi na timu pinzani ikitushambulia, laini ikiwa inajilinda huwa tunapata tabu. Unahitaji ubora wa aina tofauti ili kucheza na kupata matokeo dhidi ya timu 'inayopaki basi', muda mwingi watakuruhusu kukaa na mpira lakini ni ngumu kukupata nafasi," alisema Slot na kuongeza,
“Mchezo wa leo (juzi) timu zote zilijaribu kujenga mashambulizi kutoka nyuma kushambulia na hiyo ikatupa nafasi ya kufanya vizuri, unaweza ukafanya marejeo, Kila mechi tuliyocheza msimu huu katika hali hiyo, tumekuwa bora sana. Mechi nyingi za namna hiyo tumepata matokeo, isipokuwa ya Man City na Chelsea."
Hata hivyo, Gerrard alipinga kauli za Slot katika uchambuzi wake baada ya mechi, akidai kocha huyo anapaswa kuacha kulalamika hadharani na badala yake kutafuta njia ya kukabiliana na tatizo hilo.
“Anahitaji kuacha kutaja masuala sijui ya low block (Timu zinazozuia muda mwingi wa mchezo),” alisema gwiji huyo wa Liverpool kupitia TNT Sports.
“Low block imekuwepo Liverpool tangu nilipokuwa nikicheza na miaka mingi kabla yangu. Hivyo ndivyo ilivyo, timu zitajaribu kufanya kila kitu kuizuia Liverpool. Jambo muhimu ni kutafuta suluhisho. Una wachezaji wenye viwango, watumie hao kugeuza mechi za low block kuwa ushindi badala ya sare."
“Watakutana na low block tena dhidi ya Bournemouth mwishoni mwa wiki. Wanapaswa kuwa wakatili na wachezaji wakubwa lazima wajitokeze na kufunga mabao ili kushinda mechi.”
Hata hivyo, Gerrard alimpongeza Slot kwa namna alivyowafanya wachezaji wake wawe watulivu na kupata ushindi dhidi ya Marseille katika Uwanja wa Stade Velodrome ambayo ni sehemu ngumu sana kwa timu ngeni.