Kisa kipigo, Ronaldo aongea peke yake

Muktasari:
- Al-Nassr, ilikutana na Kawasaki kwenye nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa ya Asia (AFC Champions League) ambapo ilichapwa mabao 3-2 huku Ronaldo akikosa bao la dakika za jiooni baada ya kumpiga chenga kipa.
RIYADH, SAUDI ARABIA: STAA wa Al Nassr, Cristiano Ronaldo alionekana akijizuia kulia huku akiongea mwenyewe na kuonyesha ishara ya mikono baada ya Al-Nassr kuondolewa katika michuano ya Klabu Bingwa barani Asia juzi.
Al-Nassr, ilikutana na Kawasaki kwenye nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa ya Asia (AFC Champions League) ambapo ilichapwa mabao 3-2 huku Ronaldo akikosa bao la dakika za jiooni baada ya kumpiga chenga kipa.
Al-Nassr walikuwa na kikosi kilichojaa nyota, wakiwemo Sadio Mane (aliyewahi kuchezea Liverpool) na mshambuliaji wa zamani wa Aston Villa, Jhon Duran.
Lakini licha ya kupiga mashuti 21 na kumiliki mpira kwa asilimia 75, kikosi cha Ronaldo kililala kwa mabao 3-2 dhidi ya timu hiyo.
Kuondolewa katika nusu fainali kunasababisha Ronaldo kumaliza msimu mwingine bila taji lolote, huku Al-Nassr wakishika nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu ya Saudi Arabia na tayari wameondolewa pia kwenye Kombe la Mfalme.
Ronaldo, mwenye umri wa miaka 40, ameshinda taji moja pekee tangu ajiunge na Al-Nassr Desemba 2022 baada ya kuondoka Manchester United ambalo ni lile la Klabu Bingwa kwa timu za Kiarabu miezi minane baada ya kutua kwake.
Baada ya mchezo kumalizika Ronaldo alionekana akinyanyua mabega akiongea peke yake na kuonyesha ishara ya mikono kama mtu anayeelekeza kitu.
Ronaldo ambaye ana mabao 97 katika mechi 108 akiwa na Al-Nassr, baada ya mechi aliandika katika mitandao ya kijamii akisisisitiza kwamba ndoto kuna muda huwa zinahitaji kusubiri.
"Wakati mwingine ndoto hulazimika kusubiri. Najivunia timu hii na kila kitu tulichoweka uwanjani.
Asanteni mashabiki wote mlioamini na kusimama nasi kila hatua."