Kipigo hakijamshtua Enrique kuwavaa Arsenal

Muktasari:
- PSG walipoteza kwa mara ya kwanza katika Ligue 1, Jumamosi ya wiki iliyopita dhidi ya Nice ilipochapwa mabao 3-1 ikiwa nyumbani.
PARIS, UFARANSA: LICHA ya kupoteza kwa mara ya kwanza wiki iliyopita tangu kuanza kwa msimu huu, kocha wa Paris Saint-Germain, Luis Enrique, amesisitiza kwamba hajali kabisa kuhusu matokeo hayo na anaona hayana chakuamua kuelekea mchezo wao wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Arsenal.
PSG walipoteza kwa mara ya kwanza katika Ligue 1, Jumamosi ya wiki iliyopita dhidi ya Nice ilipochapwa mabao 3-1 ikiwa nyumbani.
“Lengo letu lilikuwa ni kuendeleza rekodi ya kutokufungwa, lakini imeshindikana. Yote kwa yote hiyo haibadilishi lengo letu la kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa.”
PSG itakutana na Arsenal ambayo imeitoa Real Madrid ili kufika kwenye nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa kwa ushindi wa jumla wa mabao 5-1.
Alipoulizwa kama anahofia matokeo dhidi ya Nice yanaweza kuathiri chochote kuelekea mechi hii, Enrique alisema: ”Najiandaa moja kwa moja na mechi ya Jumanne ya kule London na mechi ya marudiano. Katika mechi hii tulikuwa na kama nafasi 30 za kufunga, Sijali kabisa. Tulishambulia, hatukuwaza sana, na tukakutana na kipa aliyecheza vyema na kuokoa michomo, sisi ndio timu bora zaidi Ufaransa kwa sasa na tumethibitisha hilo. Kwa sasa tunachofikiria ni kushinda Ligi ya Mabingwa.
“Nafahamu wachezaji wanaweza kuathiriwa na matokeo haya, tulistahili kushinda, hakuna shaka kuhusu hilo. Lakini mpinzani wetu alikuwa na ufanisi wa asilimia 100.”