Kipa Senegal auawa na watekaji baada ya familia kushindwa kulipa fedha za fidia
Muktasari:
- Wizara ya Uunganishaji wa Afrika na Mambo ya Nje ya Senegal, imetoa tamko juzi Jumamosi Oktoba 18, 2025 kuthibitisha kifo cha mlinda mlango huyo kijana, ambaye alipatikana amefariki nchini Ghana.
Jamii ya soka nchini Senegal, imo katika majonzi kufuatia mauaji ya golikipa chipukizi mwenye umri wa miaka 18, Cheikh Toure, ambaye aliuawa kikatili na watekaji baada ya familia yake kushindwa kukusanya fedha za kumkomboa.
Wizara ya Uunganishaji wa Afrika na Mambo ya Nje ya Senegal, imetoa tamko juzi Jumamosi Oktoba 18, 2025 kuthibitisha kifo cha mlinda mlango huyo kijana, ambaye alipatikana amefariki nchini Ghana.
Cheikh alikuwa amefunzwa katika kituo cha Esprit Foot Yeumbeul, alitekwa nyara baada ya kudanganywa na kundi la majambazi waliokuwa na silaha, waliomfanya aamini kwamba alikuwa anakwenda kushiriki majaribio ya kujiunga na klabu ya soka ya kulipwa.
Mpango huo wa kitapeli uligeuka kuwa mtego ambapo Cheikh alishikiliwa mateka, huku watekaji wakitaka fidia kutoka kwa familia yake ili kumuachia huru.
Kwa bahati mbaya, juhudi za familia hazikufanikiwa, na wahalifu hao walitekeleza tishio lao kwa kumuua kijana huyo.
Mamlaka za Senegal zimeanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo kwa kushirikiana na polisi wa Ghana. Kikosi kazi cha pamoja kinalenga kubaini mazingira kamili ya tukio hilo la kusikitisha.
Mwili wa Cheikh uko katika mchakato wa kusafirishwa kurejeshwa Senegal, kwa mujibu wa taarifa ya French Football Weekly.
Katika taarifa kwa umma, msemaji wa wizara hiyo ameeleza namna walivyopokea tukio hilo kwa masikitiko makubwa na kuipa pole familia yake huku ikielezwa uchunguzi huo unafanywa kwa umakini na kipaumbele cha juu zaidi.
Vilevile, mamlaka zimezitaka klabu, wazazi na walezi kuwa waangalifu zaidi wanapopokea ofa zisizothibitishwa za majaribio au uhamisho wa wachezaji nje ya nchi.
Taarifa hiyo pia imesisitiza kuwa wanamichezo vijana nchini Senegal wanapaswa kupitia njia rasmi na kupata taarifa kutoka kwa mamlaka za michezo kabla ya safari yoyote.
Kifo cha Cheikh kinakuja wiki chache baada ya mlinda mlango kijana nchini Hispania kufariki kutokana na pigo alilopata kichwani wakati wa mechi ya ligi.
Raul Ramirez Osorio, mwenye umri wa miaka 19, alipewa huduma ya kupumua kwa mdomo na kocha wake, na kuamshwa na mwanafunzi wa uuguzi aliyekuwa akitazama mechi, baada ya kupata mshtuko wa moyo uwanjani mwezi Septemba 2025.
Alikimbizwa hospitalini Marques de Valdecilla katika jiji la kaskazini la Santander, akiwa katika hali mbaya. Hata hivyo, ilithibitishwa kwamba alifariki dunia siku mbili baada ya kulazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi.
Tukio hilo lilitokea katika dakika ya 60 ya mechi wakati Raul aliporuka kuokoa mpira wa krosi na kugongana na mshambuliaji wa timu pinzani.
Kocha wake Rafa de Pena alikimbia uwanjani alipomwona kijana huyo akianguka na kupoteza fahamu, na kwa msaada wa mwanafunzi wa uuguzi, walifanikiwa kumrudisha katika hali nzuri, lakini mshtuko wa moyo wa pili alioupata njiani kuelekea hospitalini ulizidisha hali yake kuwa mbaya na kusababisha kifo chake. Mechi hiyo ilisimamishwa mara moja baada ya tukio hilo.
Wakati huohuo, wachezaji watatu vijana wa kriketi nchini Afghanistan wameuawa katika shambulio la anga lililodaiwa kufanywa na jeshi la Pakistan katika jimbo la Paktika.
Waathiriwa hao ni Kabeer Agha, Sibghatullah, na Haroon walikuwa miongoni mwa raia wanane waliouawa na wengine saba kujeruhiwa baada ya mashambulio ya ndege zisizo na rubani kupiga wilaya ya Urgun siku ya Ijumaa, Oktoba 17, 2025. Mashambulio hayo yalivunja makubaliano ya kusitisha vita kwa saa 48 kati ya nchi hizo mbili.
Wachezaji hao walikuwa wakirejea kutoka kwenye mechi ya kirafiki huko Sharana, mji mkuu wa Paktika, waliposhambuliwa wakati wa mkusanyiko.
Bodi ya Kriketi ya Afghanistan (ACB) imelaani shambulio hilo na kuliita kama kitendo cha kigaidi kilichofanywa na utawala wa Pakistan.
Pia imetangaza kujiondoa kwenye mfululizo wa michezo dhidi ya Pakistan na Sri Lanka iliyopangwa kufanyika Lahore na Rawalpindi kuanzia Novemba 17 hadi 29, 2025, kama ishara ya heshima kwa waathiriwa.
Bodi hiyo imesema: “Bodi ya Kriketi ya Afghanistan inaeleza huzuni na masikitiko makubwa juu ya kifo cha kishujaa cha wachezaji wetu wa kriketi kutoka Wilaya ya Urgun, Jimbo la Paktika, waliolengwa jioni hii katika shambulio la kigaidi lililofanywa na utawala wa Pakistan.”