Kipa Lammens apewa mchongo wa Anfield
Muktasari:
- Hasa ukizingatia kwamba Liverpool imepoteza mechi tatu tu kati ya 83 za Ligi Kuu England ilizocheza kwenye uwanja wake huo katika kipindi cha misimu mitano.
LIVERPOOL, ENGLAND: ANFIELD ni mahali pagumu kwa makipa wengi wa timu pinzani.
Hasa ukizingatia kwamba Liverpool imepoteza mechi tatu tu kati ya 83 za Ligi Kuu England ilizocheza kwenye uwanja wake huo katika kipindi cha misimu mitano.
Lakini, kasheshe hilo la makipa analo kipa mpya wa Manchester United, Senne Lammens, atakayekwenda Jumapili hii uwanjani hapo kukabiliana na Liverpool kwenye mchezo wa Ligi Kuu England.
Kipa huyo Mbelgiji, Lammens, 23, ambaye alicheza mechi yake ya kwanza kwenye ushindi wa 2-0 dhidi ya Sunderland kabla ya mapumziko ya kupisha mechi za timu za taifa, anajiandaa kuwapo golini uwanjani Anfield katika kukabiliana na Liverpool yenye washambuliaji hatari akiwamo Mohamed Salah na Alexander Isak.
Lakini, kipa mwenzake Lammens kwenye kikosi cha Ubelgiji, Thibaut Courtois, anayedakia Real Madrid, amempa ujanja na kumweleza hali ilivyo atakapokwenda Anfield.
Kipa huyo wa zamani wa Chelsea, Courtois, 33, alisema: “Ni uwanja mgumu. Pengine ninachoweza kumwambia atakapoenda hapo awapigie makofi mashabiki wa timu mwenyeji!”
Kumekuwa na utamaduni wa mashabiki wa Liverpool kuwapigia makofi makipa wa upinzani.
Mashabiki wa Liverpool wana kelele sana uwanjani kwao kitu ambacho kipa Lammens anapaswa kukitambua mapema kabla ya mchezo huo.
Kiwango cha kipa huyo kilivutia mashabiki wa Man United kwenye mchezo uliopita uwanjani Old Trafford, ambapo walikuwa wakiimba nyimbo za kutaja jina lake na kumfananisha na kipa wao mahiri wa zamani, Peter Schmeichel.
Lammens anapewa nafasi kubwa ya kuanza katika mchezo huo baada ya Altay Bayindir kufanya makosa mengi katika mechi za mwanzoni mwa msimu. Courtois amekuwa akiamini katika ubora wa kipa Lammens mwenye kimo cha futi 6 na inchi 4, huku akifanya mambo yake kwa kujifunza kwa makipa mahiri kama Courtois, Marc-Andre ter Stegen, Manuel Neuer na Simon Mignolet.