Kauli ya Lisandro Martinez yamchekesha Carragher

Muktasari:
- Carragher alisema kwamba hakuna kilichomvunja mbavu kwa kicheko kama kusikia maneno ya beki wa Man United, Lisandro Martinez kwamba kwa sasa wana akili mpya baada ya kupata matokeo ya sare kwenye mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Liverpool uwanjani Anfield.
LONDON, ENGLAND: UKICHOKA watu wanakuchoka zaidi. Na hicho ndicho kinachotokea Manchester United baada ya gwiji wa wapinzani wao Liverpool, Jamie Carragher kuwapiga kijembe kwamba wachezaji wa Mashetani Wekundu hao wa Old Trafford wanamchekesha tu ukisikia wanachosema.
Carragher alisema kwamba hakuna kilichomvunja mbavu kwa kicheko kama kusikia maneno ya beki wa Man United, Lisandro Martinez kwamba kwa sasa wana akili mpya baada ya kupata matokeo ya sare kwenye mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Liverpool uwanjani Anfield.
Man United ilimchukua kocha Ruben Amorim kutoka Sporting Lisbon, Novemba mwaka jana kuja kurithi mikoba ya Erik ten Hag, aliyefunguliwa mlango wa kutokea baada ya timu hiyo kupata matokeo ya hovyo uwnajani.
Lakini, Mreno Amorim ambaye anaaminika kuwa mmoja wa makocha wanaoibukia kwa kasi Ulaya bado anapambana na hali yake kubadilisha hali ya mambo Old Trafford kutokana na timu hiyo kuendeleza matokeo mabovu.
Man United imevuna pointi 11 katika mechi 11 ilizocheza Ligi Kuu England tangu Amorim alipojiunga baada ya kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa Brighton, Jumapili iliyopita. Na Carragher amewashambulia wachezaji baada ya kocha huyo kukiri kwamba kikosi hicho kina wachezaji wa hovyo zaidi kuwahi kutokea kwenye historia.
Baada ya kuhoji kauli ya Amorim, Carragher alisema: “Wala siwahurumii wachezaji wa Man United, kwa sababu wamekuwa vichekesho kwa miaka ya karibuni.
“Wiki chache zilizopita walipocheza na Liverpool kuna mchezaji Lisandro Martinez alihojiwa na kudai kwamba wametumia akili huko akionyesha kidole chake kichwani. Nilikaribia kuvunja mbavu kwa kicheko kwa kile nilichokuwa nakiona, kwa sababu mara nyingi tu, Man United imekuwa ikicheza kwa kiwango cha hovyo kwa miaka minne au mitano iliyopita.
“Kuhusu ile kauli ya kocha, napata shida sasa atawezaje kwenda vyumbani kuwahamasisha wachezaji wake wapambane na kuwajenga kuwa na imani kama anawaambia wao ni kikosi kibovu zaidi kuwahi kutokea kwenye historia ya Manchester United.
“Nitashangaa kama mabosi wa Man United watashinda kumwambia kitu Amorim. Kocha wa Man United huwezi kuzungumza vitu kama vile. Huwezi kumwagia petroli kwenye moto.”
Man United kwa sasa ipo kwenye 10 la chini kwenye msimamo wa Ligi Kuu England baada ya kushindwa kurudi kwenye viwango vyao baada ya uanza msimu vibaya chini ya Ten Hag, ambaye alipigwa kibuti Oktoba jana, miezi michache tangu asainishwe mkataba mpya.
Miamba hiyo inashika nafasi ya 13 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, pointi 10 juu ya timu zinazopambana vita ya kukwepa kushuka daraja na Carragher alisema Amorim maneno yake ni kitu cha hovyo kuwahi kuzungumzwa na kocha kwa wachezaji wanaojaribu kujitafuta.
“Kwanini unasema maneno kama yale - maneno kama yale yanasemwa na wachambuzi, mtu kama mimi, yeye anapaswa kuwatetea wachezaji wake. Sifahamu analenga kupata nini, kuna faida gani atapata,” alisema Carragher.
“Sote tunafahamu kwamba Man United ni mbovu. Imepoteza mechi nyingine nyumbani dhidi ya Brighton, wamekuwa wakifanya hivyo kwa miaka kadhaa sasa. Tunajua huu ni msimu wao mgumu, tunajua timu yao ni mbovu. Anapaswa kulainisha mambo. Hii kauli yake itamshambulia hadi mwisho wa msimu.
“Amewaambia waandishi wa habari pale, ‘nawapa kichwa cha habari’. Kwanini afanye vile kama kocha, Mimi sijaelewa.”