Gyokeres kasema kitu Arsenal ikimtaka

Muktasari:
- Gyokeres, 26, alifunga bao lake la 53 msimu huu, Jumamosi iliyopita na kuisaidia Sporting Lisbon kunyakua ubingwa wa Primeira Liga.
LISBON, URENO: STRAIKA, Viktor Gyokeres amevunja ukimya baada ya Arsenal kumfanya kuwa chaguo la kwanza kwenye usajili wa dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi.
Gyokeres, 26, alifunga bao lake la 53 msimu huu, Jumamosi iliyopita na kuisaidia Sporting Lisbon kunyakua ubingwa wa Primeira Liga.
Fowadi huyo wa kimataifa wa Sweden amekuwa akihusishwa na mpango wa kujiunga na Arsenal kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi na ripoti za kutoka Ureno ni kwamba mchezaji huyo ameshafikia makubaliano ya mambo binafsi na miamba hiyo ya Emirates.
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta anataka straika mpya kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi na Gyokeres amewekwa kwenye mpango wa kwanza katika orodha ya wachezaji inaowasaka, sambamba na straika wa RB Lezipig, Benjamin Sesko.
Gyokeres alikuwa kimya kwa karibu kwa kipindi chote ambacho jina lake limekuwa likihusishwa na mpango wa kuachana na miamba hiyo ya Ureno. Lakini, sasa alisema: "Hili ni soka, bado nipo."
"Sijui nini kitakwenda kutokea. Hakuna mwenye uwezo wa kujua mambo ya baadaye."
Hilo limekuja baada ya straika wa zamani wa Arsenal, Julio Baptista kufichua kwamba mkurugenzi mpya wa michezo, Andrea Berta amemuweka Gyokeres kwenye mipango yake, aliposema: "Huyu kijana yeye ni namba tu. Mechi 45, mabao 44, asisti 11. Arsenal ni moja ya timu inayopaswa kuvutiwa naye."
Rais wa Sporting, Frederico Varandas, alionekana kuchoshwa na maswali mengi ya kuhusu hatima ya mshambuliaji huyo, aliposema: "Gyokeres alikuwa anaondoka mwaka jana, mwaka mmoja uliopita, kila siku Gyokeres anaondoka, Gyokeres anaondoka, haya sasa. Sisi ni mabingwa na Gyokeres ameshaondoka."
Arsenal ina majina ya mastraika wengine kadhaa ubaoni ambao inaweza kuwanasa ikishindwa kumsajili Gyokeres, ambao ni pamoja na Sesko, Liam Delap na Alexander Isak.