Kanuni ya Embiid kutibua ndoto ya Doncic kuwa MVP?
Muktasari:
- Hata hivyo, pamoja na takwimu zake za kuvutia, jina lake halionekani katika orodha za wanaowania tuzo ya ‘Most Valuable Player’ (MVP), jambo lililozua maswali mengi miongoni mwa wachambuzi na mashabiki. Swali linaloulizwa ni je, ni kanuni ipi inaweza kumzuia kushinda u-MVP wake wa kwanza akiwa na Los Angeles Lakers?
LOS ANGELES, MAREKANI: LUKA Doncic ameuanza msimu mpya wa Ligi ya Kikapu Marekani (NBA) kwa kiwango bora akipambana kuonyesha kiwango ambacho kimeanza kumtofautisha na wachezaji wengi katika ligi.
Hata hivyo, pamoja na takwimu zake za kuvutia, jina lake halionekani katika orodha za wanaowania tuzo ya ‘Most Valuable Player’ (MVP), jambo lililozua maswali mengi miongoni mwa wachambuzi na mashabiki. Swali linaloulizwa ni je, ni kanuni ipi inaweza kumzuia kushinda u-MVP wake wa kwanza akiwa na Los Angeles Lakers?
DONCIC NA LAKERS
Lakers imeanza msimu vizuri ikiwa na rekodi ya ushindi wa mechi saba na vipigo viwili kuelekea mchezo dhidi ya Atlanta Hawks, jambo linaloiweka karibu na nafasi ya kuwania ubingwa wa Kanda ya Magharibi (Western Conference).
Lakini, katika michezo tisa ya mwanzo, Doncic amecheza mitano kutokana na maumivu ya mguu wa kushoto na utaratibu wa kupumzishwa kimkakati uliowekwa na benchi la ufundi ikiwa ni hatua ya tahadhari ambayo inalenga kumlinda kwa msimu mrefu unaokuwa na mechi 82, lakini pia kutoiweka hatarini nafasi yake ya kushinda tuzo ya MVP ikizingatiwa kwamba kuna kanuni inayotaka staa anayeshinda tuzo hiyo awe amecheza michezo 65, maarufu kama ‘Kanuni ya Joel Embiid’.
CHANZO CHA KANUNI
Kanuni hiyo iliwekwa na NBA Oktoba 2023 kama hatua ya kupunguza tatizo la wachezaji bora kupumzishwa mara kwa mara bila majeraha makubwa, jambo lililojulikana kama load management yaani ni njia ya timu kujaribu kuhakikisha mchezaji yupo kwenye hali bora kimwili wakati wa michezo muhimu hususan ya mtoano (playoffs). Kwa mujibu wa kanuni hiyo, mchezaji hatashinda tuzo binafsi kama MVP, Mchezaji Bora wa Ulinzi au kuchaguliwa kwenye All-NBA Team iwapo hatacheza angalau michezo 65 ya msimu wa kawaida.
Kamishna wa NBA, Adam Silver aliwahi kuelezea, “hakuna uchawi katika idadi ya mechi 65, lakini tunatambua kuna michezo ambayo mchezaji anaweza kukosa kutokana na majeraha au mapumziko
JORDAN ANA HOJA?
Wakati flani mkongwe wa mpira wa kikapu duniani, Michael Jordan aliwahi kuikosoa tabia ya wachezaji kupumzishwa mara kwa mara akisema: “Sikuwahi kutaka kukosa mchezo wowote. Kila mchezo ulikuwa fursa ya kuthibitisha kwa mashabiki waliolipa pesa zao kuniona nikicheza.” Kauli hiyo inaonyesha mtazamo wa zamani wa ushindani uliotawaliwa na nidhamu na kujituma ikilinganishwa na kizazi cha sasa kinacholindwa na utaratibu wa kiafya na mikataba mikubwa.
MFANO WA EMBIID
Kanuni hiyo ilipewa jina lisilo rasmi la ‘Kanuni ya Joel Embiid’ kutokana na historia ya nyota huyo wa Philadelphia 76ers aliyeshinda tuzo ya NBA MVP msimu wa 2022-23 baada ya kutawala kwa wastani wa alama 33.1 na ribaundi 10.2.
Lakini, katika misimu miwili iliyofuata alicheza michezo 39 ya msimu mrefu na kisha 19 ya ule mdogo na hivyo akapoteza sifa ya kushindania tena tuzo hiyo.
DONCIC UWANJANI
Tangu ajiunge na NBA 2018 akiwa wa tatu katika drafti, Doncic amekuwa akicheza kati ya michezo 60 hadi 70 kwa msimu.
Alianza kwa nguvu akiwa na Dallas Mavericks akicheza michezo 72 na kushinda tuzo ya ‘Rookie of the Year’ 2018-19.
Lakini, msimu uliopita alipochezea timu mbili za Mavericks na Lakers, alicheza michezo 50 akishindwa kufikia kiwango kinachohitajika. Msimu wa 2019-20 aliwahi kucheza chini ya mechi 65, huku ule wa 2021-22 akicheza michezo 65, lakini akionyesha kiwango cha chini kutostahili tuzo.
Kwa sasa, Doncic anaonekana kuwa mchezaji bora zaidi duniani anapokuwa uwanjani, lakini changamoto ni kuhakikisha anakomaa uwanjani vya kutosha. Kucheza michezo 65 inaweza kuonekana kuwa jambo dogo, lakini kwa mchezaji anayepumzishwa kimkakati kutokana na majeraha au uchovu ni changamoto.
Lakers wana nia ya kumlinda nyota wao huyo wa thamani kubwa hasa baada ya kusaini mkataba wa miaka mitatu wenye thamani ya Dola 165 milioni, lakini kupumzishwa kupita kiasi kunaweza kumgharimu tuzo ya kihistoria.
UPO MJADALA
Wapo mashabiki wanaoamini kwamba kanuni hiyo inaleta usawa na kuwapa mashabiki thamani ya fedha zao, lakini wengine wanaamini kwamba inawaadhibu wachezaji wanaojitunza kiafya kwa manufaa ya timu zao. Kwa hali ilivyo sasa, ndoto ya Doncic kushinda MVP akiwa na Lakers ipo mikononi mwa idadi ya michezo atakayocheza na si ubora wake uwanjani. Ikiwa atafikia kizingiti cha michezo 65, ulimwengu wa NBA huenda ukashuhudia historia mpya.