Kane awapiga bao Ronaldo, Haaland
Muktasari:
- Nahodha huyo wa timu ya taifa ya England alitikisa nyavu mara mbili katika ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Werder Bremen, na kufikia rekodi hiyo katika mechi 104 tu tangu ajiunge na Bayern mwaka 2023 akitokea Tottenham.
MUNICH, UJERUMANI: MSHAMBULIAJI wa Bayern Munich, Harry Kane ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga mabao 100+ ndani ya mechi chache zaidi akiwa na klabu ya Ligi tano bora barani Ulaya.
Nahodha huyo wa timu ya taifa ya England alitikisa nyavu mara mbili katika ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Werder Bremen, na kufikia rekodi hiyo katika mechi 104 tu tangu ajiunge na Bayern mwaka 2023 akitokea Tottenham.
Kane amewazidi Cristiano Ronaldo (Real Madrid) na Erling Haaland (Manchester City) waliowahi kufikia idadi hiyo mabao baada ya kucheza mechi 105.
Staa huyu ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 32, yupo kwenye kiwango bora sana msimu huu na hadi sasa amefunga jumla ya mabao 15 katika mechi nane tu.
Bao lake la kwanza lilitokana na penalti kabla ya kufunga jingine katika dakika ya 65, kisha kutolewa katika dakika ya 77 huku mashabiki wa Allianz Arena wakimpa heshima ya kusimama.
Mabao ya Jonathan Tah na Konrad Laimer pia yaliisaidia Bayern kuendeleza rekodi ya ushindi wa 100 msimu huu katika Bundesliga na kujikita zaidi kileleni ikiwa na pointi tano mbele ya Borussia Dortmund.
Akizungumzia rekodi hiyo baada ya mechi, Kane alisema: “Ni kitu kizuri kwangu. Ni heshima kubwa kufikisha mabao 100 katika klabu hii kubwa. Hii pia imetokana na msaada kutoka wachezaji wenzangu na benchi la ufundi, nina matumaini ya kufunga mengine 100 zaidi.”
Kane alijiunga na Bayern akitokea Tottenham kwa dau kubwa la Pauni 104 milioni mwaka 2023 na katika msimu wake wa kwanza, alifunga mabao 44 na kutoa pasi 12 za mabao.
Msimu uliofuata, alifunga mabao 41 na kutoa pasi 14 katika mechi 51 za michuano yote alizocheza.
Licha ya rekodi hizo kubwa za mabao, staa huyu wiki hii alimaliza katika nafasi ya 13 kwenye kinyang’anyiro cha kuwania tuzo ya Ballon d’Or ya Mwanasoka Bora wa Dunia iliyochukuliwa na Ousmane Dembele wa PSG.