Juventus yaongoza mbio za kumuwania nyota Greenwood Marseille
Muktasari:
- Tangu wakati huo mchezaji huyo aliyekuzwa katika viunga vya Old Trafford amechezea Getafe (Hispania) na sasa Marseille ya Ufaransa, ambako kote ameng’ara na kuvutia vigogo vingi vya soka Ulaya vinavyotamani kuwa naye katika vikosi.
MARSEILLE, UFARANSA: KINACHOELEZWA ni kwamba Mason Greenwood ameanza kuivutia Manchester United kumrejesha kikosini baada yab kuachana naye misimu mitatu iliyopita, kufuatia kasha ya kumpiga mpenziwe na kusababishia majeraha yaliyompa kesi ya unyanyasaji wa kijinsia huko England.
Tangu wakati huo mchezaji huyo aliyekuzwa katika viunga vya Old Trafford amechezea Getafe (Hispania) na sasa Marseille ya Ufaransa, ambako kote ameng’ara na kuvutia vigogo vingi vya soka Ulaya vinavyotamani kuwa naye katika vikosi.
Lakini, akiwa sasa ameanza kutuliza presha huko Marseille na akiongoza katika msimamo wa wafungaji wa Ligi Kuu Ufaransa kwa mabao 15, ofa zimeanza kumfuata upya akiwa kinara wa washambuliaji ambao mwisho wa msimu huu watakuwa katikati ya mjadala wa wapi ataibukia msimu ujao.
Kwa Manchester United hata kama itashindwa kumrudisha, lakini inaweza kunufaika kifedha kutokana na ada ya Pauni 43 milioni atakayonunuliwa kwani ina mgawo wa karibu asilimia 40 katika mauzo.
Sehemu ya ada hiyo ya uhamisho itaenda Manchester United ambao wana kipengele cha kunufaika na uhamisho wa baadaye (sell-on clause) baada ya kumuuza kwa Pauni 30 milioni kwenda klabu hiyo ya Ufaransa Julai 2024.
Greenwood anaweza kubadili klabu mwisho wa msimu, huku mshambuliaji huyo akihusishwa na kujiunga na moja ya klabu kubwa Ulaya, lakini Juventus ndiyo inayotawala kwa sasa katika mijadala mbalimbali inayoendelea kumhusu mchezaji huyo. Kwa ujumla amefunga mabao 25 katika mechi 38 kwenye mashindano yote hadi sasa huko Marseille pamoja na kutoa asisti nane.
Kwa mujibu wa La Gazzetta dello Sport, Marseille huenda wakalazimika kumuuza Greenwood kwa sababu za kifedha iwapo watashindwa kufuzu Ligi ya Mabingwa msimu ujao, wakiwa nafasi ya tatu katika Ligue 1 na pointi 49 - mbili mbele ya Lyon walio nafasi ya nne, tatu mbele ya Lille walio nafasi ya tano, na sita mbele ya Monaco na Rennes walio nafasi ya sita na saba. Timu tatu za juu Ligue 1 hufuzu Ligi ya Mabingwa moja kwa moja msimu ujao.