Jose Mourinho anaondoka muda wowote
Muktasari:
- Mourinho, mwenye miaka 62, alikuwa huru baada ya kufutwa kazi na Fenerbahce mwezi uliopita kufuatia kushindwa kwao kufuzu Ligi ya Mabingwa, kabla ya kutangazwa rasmi kama kocha mkuu wa Benfica Alhamisi alasiri.
LISBON, URENO: BAADA ya kusaini mkataba wa miaka miwili wa kuitumikia Benfica, taarifa za ndani zinaeleza kocha Jose Mourinho huenda akaondoka mwishoni mwa msimu huu kutokana na vipengele vilivyopo.
Mourinho, mwenye miaka 62, alikuwa huru baada ya kufutwa kazi na Fenerbahce mwezi uliopita kufuatia kushindwa kwao kufuzu Ligi ya Mabingwa, kabla ya kutangazwa rasmi kama kocha mkuu wa Benfica Alhamisi alasiri.
Benfica ilithibitisha uteuzi huo ikisema kuna makubaliano ya kumsainisha Mourinho mkataba utakaodumu hadi mwisho wa msimu wa 2026-27.
Katika mkataba kimewekwa kipengele kinachoelezea ni kiasi gani ambacho Mourinho atatakiwa kulipwa endapo atafutwa kazi.
Vilevile kinaeleza kama Mourinho ataamua kujiuzulu atalazimika kulipa kiasi sawa na kile ambacho klabu inatakiwa kumlipa endapo itamfukuza kazi.
Katika mkutano wake wa kwanza na wanahabari, Mourinho alizungumza ajira yake hiyo mpya na kueleza matarajio yake.
“Kazi yangu ni kubwa, nimefundisha timu katika nchi mbalimbali, nilifanya uamuzi mbaya katika baadhi ya maeneo na nilifanya uamuzi mzuri pia, lakini sina majuto. Najua tulichofanya vizuri na tulichokosea. Nilifanya kosa kwenda Fenerbahce, lakini nilijitolea mpaka siku ya mwisho. Kufundisha Benfica naona kama nimerudi katika kiwango changu.”
“Ahadi zina thamani yake. Wakati ule nikiwa FC Porto, niliahidi na nilifanya kile nilichoahidi. Naamini kwa dhati Benfica ina kila kitu cha kushinda ubingwa.” “Wamepoteza pointi mbili, na bila shaka tutapoteza zaidi ya hapo ingawa naamini si nyingi lakini tunaanza upya.”
“Benfica ina uwezo wa kutwaa ubingwa kwa wachezaji waliopo sasa. Sifichi hilo. Sio ahadi, bali ni imani kuwa tunaweza na tunapaswa kufanya hivyo.”
Mourinho, ambaye aliwahi kuinoa Benfica kwa mechi 10 mwaka 2000 kabla ya kuondoka kutokana na mabadiliko ya uongozi wa bodi na kujiunga na Uniao de Leiria ana historia nzuri sana ndani ya Ureno kwani akiwa na FC Porto alishinda ubingwa Ligi ya Mabingwa Ulaya na Ligi Kuu Ureno.