John Obi: Arsenal inacheza ‘soka haramu’
Muktasari:
- Mikel alitoa kauli hiyo wakati akizungumza kwenye kituo cha redio cha talkSPORT, ambapo alimkosoa kocha wa Arsenal, Mikel Arteta kwa kuifanya timu yake kutegemea zaidi mipira ya kona badala ya kucheza soka la kuvutia.
LONDON, ENGLAND: KIUNGO wa zamani wa Chelsea, John Obi Mikel ameishambulia vikali Arsenal akidai timu hiyo inacheza “soka haramu” na haistahili kuwa bingwa wa Ligi Kuu England msimu huu.
Mikel alitoa kauli hiyo wakati akizungumza kwenye kituo cha redio cha talkSPORT, ambapo alimkosoa kocha wa Arsenal, Mikel Arteta kwa kuifanya timu yake kutegemea zaidi mipira ya kona badala ya kucheza soka la kuvutia.
Kwa mujibu wa takwimu za Arsenal, timu hiyo imefunga mabao 21 kupitia mipira ya adhabu ya kona kwenye ligi msimu huu, zaidi ya klabu yoyote, huku mabao 35 tu kati ya 100 waliyofunga kwenye mashindano yote ndio yalitokana na mipira ya wazi.
“Ukitazama Arsenal kwa sasa wanategemea kona pekee. Umetumia karibu Pauni 1 bilioni kujenga kikosi, halafu unaniambia njia pekee ya kushinda ni kupitia kona? Hicho ni kitu cha ajabu. Wanashinda kwa namna mbaya sana.”
Aliongeza kuwa hata mashabiki wa Arsenal wasingefurahia aina hiyo ya mchezo ikiwa timu yao isingekuwa inaongoza msimamo wa ligi.
“Sababu pekee mashabiki hawalalamiki ni kwa sababu wako juu ya ligi. Kama wasingekuwa juu, mashabiki wangelalamika kwamba hawafurahii aina ya soka wanalocheza,” alisema.
Obi pia alidai mbinu za Arsenal kwenye mipira ya kona si halali kwa sababu wachezaji wanazuia makipa na kuwashika wapinzani wao ili kuzuia wasiruke.
“Kwangu mimi hiyo ni haramu. Wachezaji wanamzuia kipa na pia wanawazuia wengine kuruka. Niliona kwenye mechi dhidi ya Chelsea, Declan Rice alikuwa anamshika beki wa kushoto Jorrel Hato.”
Hata hivyo, Arsenal si timu pekee inayokosolewa kwa kutumia nguvu kwenye mipira ya kona kwani suala hilo limekuwa likijadiliwa sana kwenye ligi.
Kwa mfano, Everton iliwahi kukosolewa baada ya wachezaji wao kumzonga kipa wa Manchester United, Senne Lammens wakati wa kupiga kona mwezi uliopita.
Kocha wa Liverpool, Arne Slot naye amewahi kusema kuwa mechi nyingi za sasa si za kufurahisha kutokana na mbinu hizo za mipira ya kutengwa.