Joey Barton ashtakiwa tena kwa kujeruhi
Muktasari:
- Polisi wa Merseyside wamethibitisha kwamba Barton pamoja na Gary O’Grady (50), wameshtakiwa kufuatia madai ya shambulio lililotokea Huyton usiku wa Jumapili iliyopita.
MERSEYSIDE, ENGLAND: BAADA ya kuandamwa na mikasa mbalimbali ya nje ya uwanja iliyomfikisha mahakamani, nyota wa zamani wa kimataifa wa England, Joey Barton, 43, ameshtakiwa kwa kosa la kujeruhi kwa nia baada ya mwanaume mmoja kupatikana akiwa na majeraha makubwa karibu na klabu ya gofu huko Liverpool
Polisi wa Merseyside wamethibitisha kwamba Barton pamoja na Gary O’Grady (50), wameshtakiwa kufuatia madai ya shambulio lililotokea Huyton usiku wa Jumapili iliyopita.
Habari hizo zinakuja baada ya Daily Mail kupitia kitengo chake cha michezo kuripoti kuwa Barton, aliyewahi kuchezea Manchester City na Newcastle United, alikuwa mmoja wa watu waliodaiwa kuhusika katika ugomvi karibu na Klabu ya Gofu ya Huyton and Prescot kwenye Wilaya ya Merseyside.
Huduma ya dharura iliitwa Jumapili usiku baada ya taarifa za shambulio, ambapo mwanaume mmoja alipelekwa hospitali kufanyiwa uchunguzi wa majeraha kwenye uso na mbavu.
Inaelezwa kuwa mwanaume aliyejeruhiwa ni Kevin Lynch (51), baba wa watoto wawili, ambaye anadaiwa kushambuliwa na Barton katika klabu hiyo. Barton alifikishwa mahakamani ambapo alinyimwa dhamana na kuamriwa abaki rumande kwa mwezi mmoja. Inaaminika kuwa mabishano yalianza ndani ya jengo la klabu, na baadaye kuna madai kwamba silaha ililetwa kutoka nje ya jengo hilo. Katika taarifa yake, Polisi wa Merseyside walisema: “Sasa tunaweza kuthibitisha kuwa wanaume wawili wameshtakiwa kufuatia shambulio lililotokea Huyton usiku wa Jumapili, Machi 8. Saa 3 usiku huduma za dharura ziliitwa Fairway kufuatia taarifa za mwanaume kushambuliwa karibu.
“Mwathiriwa alipelekwa hospitali kwa ajili ya tathmini ya majeraha makubwa kwenye uso na mwili. Kwa sasa yuko hospitalini katika hali mbaya.”
Katika kesi nyingine Mahakama Kuu ya England kuhusu kashfa inayomhusu Barton ililazimika kuahirishwa kwa kuwa hakuwapo kutoka na kuwa mahabusu.