Joe Cole: Bruno Man United wasikuzingue sana

Muktasari:
- Fernandes amefunga mabao 16 na kutoa asisti 15 kwa msimu huu licha ya Man United kutokuwa na mwendelezo wa matokeo mazuri.
MANCHESTER, ENGLAND: LEJENDI wa Chelsea, Joe Cole amemshauri kapteni wa Manchester United, Bruno Fernandes kuachana na timu hiyo katika dirisha lijalo na kujiunga na timu nyingine itakayomwezesha kupata mafanikio zaidi.
Fernandes amefunga mabao 16 na kutoa asisti 15 kwa msimu huu licha ya Man United kutokuwa na mwendelezo wa matokeo mazuri.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30 alifunga hat-trick muhimu dhidi ya Real Sociedad iliyoisaidia Man United kufika nusu fainali ya Europa League.
Hata hivyo, Fernandes amekuwa akikosolewa sana na malejendi wa timu hiyo hususani kapteni wa zamani Roy Keane kuhusu uongozi wake.
Cole amesema Fernandes lazima ajisikie kukwazika kutokana na ukosoaji anaopata licha ya kuwa ni mchezaji anayeisaidia sana Man United msimu huu.
Kiungo huyu wa zamani wa Chelsea na Liverpool alidai kuwa Fernandes, ambaye amefunga mabao 95 na kutoa asisti 81 katika mechi 277 za Man United, anapaswa kuhamia timu itakayomwezesha kushinda mataji.
"Kama mimi ningekuwa Bruno Fernandes, ningeondoka Manchester United. Yeye ni mtu muhimu lakini anapokea mishale kutoka kwa kila mtu," alisema Cole.
"Kuna wakati inawezekana akawa anaenda nyumbani usiku na kujiuliza ni kwa nini kila mtu anamlaumu kwamba yeye ndio tatizo.
"Kuna wengine wanacheza vizuri lakini yeye kwa kweli ndio mhimili wa timu katika kipindi hiki kigumu. Yeye ni mchezaji bora na unaweza kumuweka katika timu nyingi, na akafaulu, lakini sidhani kama ameshinda taji la ligi katika maisha yake ya soka na anahitaji kwenda kuthibitisha mwenyewe kwamba anaweza kucheza katika timu bora kwa sababu ameshamaliza kwa upande wa Man United."
"Anapaswa kuachana na timu hiyo, huenda wakampa heshima yake. Yeye ni mchezaji mzuri na kama ningekuwa mimi, ningetafuta kwenda kucheza katika timu inayoweza kushinda mataji."
Tangu alipojiunga na Man United, Fernandes ameshinda Kombe la Carabao mara moja mwaka 2023 na pia alikuwa katika kikosi kilichoshinda Kombe la FA, Mei mwaka jana.