Jesus ashikilia jezi ya Gyokeres Arsenal
Muktasari:
- Gyokeres, 27, anataka kujiunga na Arsenal kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi na sasa dili hilo lipo kwenye hatua za mwisho kukamilika.
LONDON, ENGLAND: ARSENAL haitampa straika Viktor Gyokeres jezi yenye namba ya ndoto zake wakati mkali huyo atakapokamilisha uhamisho wake wa kujiunga na miamba hiyo ya Emirates kwa dili la Pauni 63.7 milioni.
Gyokeres, 27, anataka kujiunga na Arsenal kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi na sasa dili hilo lipo kwenye hatua za mwisho kukamilika.
Makubaliano binafsi yameshafikiwa, lakini kuna vitu vidogo bado havijafikia makubaliano baina ya Arsenal na Sporting Lisbon.
Mabingwa hao wa Ureno, ambao Gyokeres aliwafungia mabao 97 katika mechi 102 hadi sasa, haijafikia makubaliano ya malipo ya bonasi ambayo Arsenal itapaswa kulipa itakapokamilisha uhamisho wa mkali huyo.
Baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya AC Milan kwenye mechi ya kirafiki huko Singapore, Arteta alisema: "Unajua siwezi kumtumia mchezaji ambaye hayupo hapa." Hiyo ni wakati alipoulizwa kuhusu dili la Gyokeres.
Arteta atakuwa na kauli nyingine juu ya straika Gyokeres wakati atakapokamilisha vipimo vya afya na kusaini mkataba wa miaka mitano. Fowadi huyo wa kimataifa wa Sweden anatazamiwa kwenda kuonyesha makali makubwa ya kufunga bao kwenye Ligi Kuu England kama ambavyo alifanya kwenye Primeira Liga.
Staa huyo amekuwa akivaa jezi yenye Namba 9 tangu alipojiunga na Sporting akitokea Coventry mwaka 2023, lakini huko Arsenal namba hiyo inavaliwa na Mbrazili Gabriel Jesus. Na sasa, atalazimika kuchukua namba nyingi.
Straika huyo wakati alipokuwa Coventry, alivaa jezi yenye Namba 17, ambayo kwenye kikosi cha Arsenal hiyo inavaliwa na Oleksandr Zinchenko, ambaye anahusishwa na mpango wa kuachana na miamba hiyo ya Emirates.
Lakini, kinachovutia ni kwamba jezi Namba 10 ipo wazi, inaweza kuwa chaguo la Gyokeres huko Arsenal, ambapo akivaa hiyo atakuwa amepita kwenye nyayo za magwiji Paul Merson, Dennis Bergkamp, Robin van Persie na Mesut Ozil.
Jezi nyingine ya kibabe ambayo ipo wazi ni Namba 14, iliyopata umaarufu baada ya kuvaliwa na Thierry Henry. Mastaa wengine wa Arsenal waliovaa jezi yenye namba hiyo ni Martin Keown, Pierre-Emerick Aubameyang, Alan Smith, Ray Parlour na Kevin Campbell.
Gyokeres alivaa jezi Namba 10 utotoni, kisha alivaa namba 12, 14, 42 na 9 kwenye soka la timu za wakubwa. Namba zote ambazo zipo wazi Arsenal ni 10, 25, 26, 34 na 35.