Jamie Redknapp: Salah aachwe Januari, lasivyo...
Muktasari:
- Redknapp ambaye alipendekeza kuwa Salah auzwe hata katika dirisha lijalo, amesema ana wasiwasi kuwa Salah na Liverpool wanaweza kuachana vibaya baada ya kuanza mechi akiwa benchini kwa mara ya pili mfululizo dhidi ya Sunderland.
LIVERPOOL, ENGLAND: MSHAMBULIAJI wa zamani wa Liverpool, Jamie Redknapp, amekiri kuwa atashangaa sana ikiwa Mohamed Salah atamaliza mkataba wake wote katika viunga vya Anfield, akidai kuwa uhusiano wa staa huyo raia wa Misri na majogoo umefika “kikomo.”
Redknapp ambaye alipendekeza kuwa Salah auzwe hata katika dirisha lijalo, amesema ana wasiwasi kuwa Salah na Liverpool wanaweza kuachana vibaya baada ya kuanza mechi akiwa benchini kwa mara ya pili mfululizo dhidi ya Sunderland.
Salah, mwenye miaka 33, aliingizwa kipindi cha pili katika mechi hiyo, lakini hakuweza kuleta tofauti katika mechi hiyo iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1.
Aprili mwaka huu Salah alisaini mkataba mpya na Liverpool wa kuendelea kusalia katika viunga hivyo hadi mwaka 2027, lakini sasa mambo yanaonekana kuwa tofauti baada ya kiwango chake kushuka.
Salah alisainishwa mkataba huo kutokana na mchango wake mkubwa katika kikosi msimu uliopita ambapo alifunga mabao 29 na kutoa asisti 18 katika mechi 38 za EPL na kuiwezesha Liverpool kutwaa taji la EPL.
Hata hivyo, sio Salah pekee anayeonekana kushuka kiwango, karibia kikosi kizima cha Liverpool kinaonekana kuwa katika kiwango cha chini jambo ambalo limeanzisha pia shinikizo kwa kocha Arne Slot ambaye baadhi ya mashabiki wanataka afukuzwe.
"Salah ni miongoni wachezaji wakubwa wa Ligi Kuu England, pia ni gwiji wa Liverpool, lakini kwa hali ya mambo ilivyo, binafsi nafikiri hili halitaisha vizuri. Nitashangaa kama atamaliza miaka miwili iliyobaki kwenye mkataba wake akiwa hapo. Kwa sasa kinachofanyika ni kama kutaka kumtupia lawama yeye, akionekana ndio anaikwamisha timu kiasi cha kuwekwa benchini. Akiondoka hata Januari hatokuwa mchezaji wa kwanza kufanya hivyo."
Mapema wiki hii, kocha Slot alikiri kuwa Salah hakufurahishwa na kukaa benchini kwenye mechi dhidi ya West Ham na akaweka wazi kwamba hakuzungumza naye kabla ya kutomwanzisha mechi dhidi ya West Ham tofauti na alivyofanya alipoamua kutomwanzisha dhidi ya Frankfurt.