AFCON 2025: Emam Ashour, Mostafa Fathi warudishwa The Pharaohs
Muktasari:
- Kocha Hossam ametangaza kikosi chake, huku kukiwa na habari njema kwa mashabiki wa “The Pharaohs”, kwani baadhi ya wachezaji muhimu waliokuwa majeruhi amewajumuisha.
Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Misri, Hossam Hassan, ametangaza kikosi chake kitakachoshiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025) zitakazofanyika nchini Morocco.
Kocha Hossam ametangaza kikosi chake, huku kukiwa na habari njema kwa mashabiki wa “The Pharaohs”, kwani baadhi ya wachezaji muhimu waliokuwa majeruhi amewajumuisha.
Miongoni mwa waliorejea kikosini ni Emam Ashour wa Al Ahly na Mostafa Fathi wa Pyramids FC, ambao wamepona majeraha na kuongeza nguvu muhimu katika safu ya kiungo na ushambuliaji kwenye kikosi cha Misri. Kurejea kwa wachezaji hao kunatazamwa kama chachu kubwa katika ubunifu na kasi ya timu kuelekea michuano hiyo mikubwa barani Afrika.
Meneja wa timu ya taifa ya Misri, Ibrahim Hassan, amethibitisha kuwa orodha ya mwisho ya wachezaji itawasilishwa rasmi kwenye Shirikisho la Soka Afrika (CAF) Desemba 11, kama kanuni za mashindano zinavyoelekeza.
Misri itaanza kampeni yake ya AFCON Desemba 22 kwa kuikabili Zimbabwe, kisha itaikaribisha Afrika Kusini Desemba 26, kabla ya kumaliza hatua ya makundi kwa mchezo muhimu dhidi ya Angola Desemba 29.
Kikosi cha Misri kilichoitwa kwa ajili ya AFCON 2025 kipo hivi;
Makipa: Mohamed El-Shenawy, Ahmed El-Shenawy, Mostafa Shobeir na Mohamed Sobhi.
Mabeki: Mohamed Hany, Ahmed Eid, Rami Rabia, Khaled Sobhi, Yasser Ibrahim, Mohamed Ismail, Hossam Abdelmaguid, Mohamed Hamdy na Ahmed Fattouh.
Viungo: Marwan Attia, Hamdy Fathy, Mohanad Lasheen, Mahmoud Saber, Mohamed Shehata, Emam Ashour, Ahmed Sayed Zizo, Mahmoud Hassan “Trezeguet,” Ibrahim Adel, Mostafa Fathi na Omar Marmoush.
Washambuliaji: Mohamed Salah, Mostafa Mohamed, Salah Mohsen na Osama Faisal.