Jamie O'Hara aibua mjadala akiitaja Arsenal
Muktasari:
- O'Hara amesema hivi, hakuna mtu atakayekumbuka timu ya Arsenal inayodaiwa kuwa “ya kuchosha zaidi” katika historia endapo itashinda taji la Ligi Kuu England msimu huu.
LONDON, ENGLAND: JE, unaweza kuyachukua maoni ya mpinzani wako na kuyapa kipaumbele? Hilo swali linalowahusu Arsenal kwa sasa kutokana na kile kilichosemwa na kiungo wa zamani wa Tottenham Hotspur, ambao ni mahasimu wao wakuu, Jamie O'Hara.
O'Hara amesema hivi, hakuna mtu atakayekumbuka timu ya Arsenal inayodaiwa kuwa “ya kuchosha zaidi” katika historia endapo itashinda taji la Ligi Kuu England msimu huu.
O'Hara, ambaye kwa sasa ni mtangazaji wa talkSPORT, aliishambulia Arsenal kufuatia ushindi wao wa mabao 4-0 dhidi ya Leeds United, Jumamosi.
Mabao kutoka kwa Martin Zubimendi, Viktor Gyokeres na Gabriel Jesus, pamoja na bao la kujifunga la Karl Darlow, yalitosha kuisaidia Arsenal kufungua pengo la pointi na kufikia saba kileleni mwa msimamo wa ligi kabla ya mechi za Jumapili.
Matokeo hayo yalimaliza msururu wa mechi tatu bila ushindi na pia yaliifanya Arsenal kushinda mechi ya ligi kwa zaidi ya bao moja kwa mara ya pili tu tangu ushindi wa 2-0 dhidi ya Brentford mwanzoni mwa Desemba, 2025.
Hata hivyo, hata baada ya kuifunga Leeds United mabao manne, O’Hara, akizungumza na Rory Jennings, aliendelea kuwakosoa Arsenal akidai kuwa hakuna atakayekumbuka kikosi hiki cha kocha Mikel Arteta endapo kama kitafanikiwa kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu England.
“Ni ya kuchosha sana!,” amesema O'Hara na kuongeza: “Hakuna mtu atakayekumbuka timu hii.
“Ukiziangalia timu za Arsenal zilizopita, Invincibles. Fikiria timu kubwa ulizowahi kuona zikishinda Ligi Kuu na ukasema: ‘Wow, hii ni timu ya kipekee’ Manchester City walioshinda ligi, Manchester United, Arsenal ya zamani waliposhinda.
“Hakuna mtu atakayekumbuka timu hii ya Arsenal. Ni ya kichovu sana!”
Jennings aliingilia mazungumzo na kusema kuna baadhi ya mashabiki wanaiita timu hii ya Arsenal ‘alama za kihistoria’ na kwamba Piers Morgan aliwataja wachezaji wanne wa sasa wa Arsenal katika kikosi chake bora cha muda wote cha Ligi Kuu England kwa upande wa Washika Bunduki hao wa London, akidai kuwa ni Jurrien Timber, Gabriel Magalhaes, Declan Rice na Bukayo Saka.
“Kihistoria?” O’Hara alijibu kwa mshangao.
Akizungumzia Morgan na kikosi chake, kiungo huyo wa zamani wa Spurs aliongeza: “Najua amekuwa hospitalini na amefanyiwa upasuaji wa sikio, lakini nadhani lazima pia amefanyiwa upasuaji wa ubongo ili kutoa upuuzi wa kiwango hicho.”
O’Hara azidi kuishambulia Arsenal akisema: “Kama watafanikiwa na kuchukua ubingwa, hongera kwao.
“Lakini, hakuna atakayekuwa anatazama tena msimu huu kwenye vile vipindi vya Sky Sports Premier League Years, sivyo?
“Hakuna atakayeurudia kutazama msimu huu. Hakutakuwa na burudani kabisa, kabisa, katika kutazama msimu ambao Arsenal wanashinda.”
O’Hara hakuacha kuikosoa Arsenal hata alipozungumza na mpigaji simu hewani, akisema: “Niseme ukweli, miaka mitatu iliyopita nilifurahia sana kuitazama Arsenal na nilidhani mlikuwa timu bora zaidi kwa mbali, mlishindwa tu kufanikisha mwisho.
“Lakini, sasa labda ninyi ni timu ya kuchosha zaidi niliyowahi kuona ikishinda taji.
“Nazungumzia timu inayoshinda ubingwa ni timu ya kuchosha zaidi nadhani niliyowahi kuitazama.”
Arsenal inapambana kubeba ubingwa wao wa kwanza wa ligi baada ya kusubiri kwa zaidi ya miaka 20. Lakini, katika harakati hizo, Arsenal inategemea pia anguko la wapinzani wake katika mbio za ubingwa, Aston Villa na Manchester City ziteleze ili kumpa nafasi kubwa ya kwenda kunyakua taji hasa baada ya wapinzani hao kuangusha pointi kwenye mechi zao za Jumapili na kuifanya Arsenal sasa kuongoza kwa tofauti ya pointi sita.