Ishu ya uwanja mpya Man United ni hivi
Muktasari:
- Machi mwaka jana, miamba hiyo ya soka England ilitangaza azma yake ya kujenga uwanja mpya utakaogharimu Pauni 2 bilioni na kuachana na ule wa Old Trafford ambao umekuwa na changamoto mbalimbali ya kimiundombinu, lakini mradi huo umekuwa ukichelewa kwa sababu kadhaa.
MANCHESTER, ENGLAND: ULE mpango wa ujenzi wa uwanja mpya wa klabu ya Manchester United umechukua sura mpya na inaelezwa kinachosubiriwa kwa sasa ni uwasilishwaji wa maombi ya mchoro wa mwisho serikalini kwa ajili ya kuanza mchakato wa ujenzi katika kipindi cha miezi 12 hadi 18 ijayo.
Machi mwaka jana, miamba hiyo ya soka England ilitangaza azma yake ya kujenga uwanja mpya utakaogharimu Pauni 2 bilioni na kuachana na ule wa Old Trafford ambao umekuwa na changamoto mbalimbali ya kimiundombinu, lakini mradi huo umekuwa ukichelewa kwa sababu kadhaa.
Baada ya kuwa gumzo kutokana na kuonekana kusuasua kwa mchakato huo wa ujenzi, mabosi wa Man United wametoa taarifa mpya kuhusu uwanja huo na kutaja muda sahihi wa kuanza kazi hiyo.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mradi wa Uwanja Mpya, Collette Roche, akizungumzia maendeleo ya mchakato huo katika mahojiano aliyofanya kwenye maonyesho ya biashara yaliyofanyika huko Ufaransa alisema: “Mpango ni katika miezi michache ijayo tutakuwa tumefikia hatua fulani muhimu kuhusu kununua ardhi tunayoihitaji ambayo itakuwa hatua kubwa katika mradi huu."
Roche pia alithibitisha itachukua miezi saba kukamilisha michoro ya mwisho ya uwanja huo.
"Tunatumia muda mwingi kushirikiana na halmashauri ya eneo husika ili kuelewa masharti na kila kitu ili kufikia wakati wa kuwasilisha maombi ya ujenzi kati ya miezi 12 hadi 18, tusiwe tunaanza upya kabisa."
Akizungumzia kampuni zitakazojenga uwanja huo, alisema: "Tupo katika mchakato wa kuhakikisha tunapata timu bora ile inayofanya kazi kwa mtindo unaofanana na wetu na iliyo tayari kwa changamoto, kisha tutathibitisha uteuzi huo na kuanza rasmi ujenzi."
Man United imekuwa kwenye mazungumzo na Kampuni ya Freightliner kwa ajili ya kununua sehemu ya ardhi itakayotumika kwenye mpango wa uwanja mpya, huku pia ikizungumza na kampuni nyingine kubwa. Mmiliki mwenza wa klabu na tajiri, Sir Jim Ratcliffe, amekuwa ndiye msimamzi mkuu wa mpango wa kuiboresha upya Old Trafford na hapo awali alisema anataka ionekane kama Wembley ya Kaskazini.