Ishu ya Rashford, Barcelona ipo hivi
Muktasari:
- Barcelona imewasilisha ombi la kumsajili Rashford kwa mkopo lenye kipengele cha kumnunua baadaye, pia katika mkataba huo, mabingwa hao wa Hispania wamekubali kulipa asilimia 100 ya mshahara wake wa Pauni 325,000 kwa wiki, jambo litakaloiokoa ManUnited na gharama ya takriban Pauni 15 milioni, malipo ya mshahara kwa msimu ujao.
BARCELONA, HISPANIA: NDOTO ya nyota wa kimataifa wa England na Klabu ya Manchester United, Marcus Rashford ya kutua Barcelona huenda ikatimia hivi karibuni baada ya miamba hiyo ya England kukubali kumtoa kwa mkopo baada ya ameambiwa hahitajiki Old Trafford.
Barcelona imewasilisha ombi la kumsajili Rashford kwa mkopo lenye kipengele cha kumnunua baadaye, pia katika mkataba huo, mabingwa hao wa Hispania wamekubali kulipa asilimia 100 ya mshahara wake wa Pauni 325,000 kwa wiki, jambo litakaloiokoa ManUnited na gharama ya takriban Pauni 15 milioni, malipo ya mshahara kwa msimu ujao.
Ingawa dili hilo bado halijakamilika rasmi, Man United imekubali kumuacha Rashford aondoke kwa mkopo na pande zote zinatarajia kukamilisha makubaliano hayo ndani ya wiki moja.
Rashford alitumia nusu ya pili ya msimu uliopita kwa mkopo Aston Villa baada ya dili la kuhamia Hispania kuvunjika Januari mwaka huu kutokana na ugumu wa mazungumzo.
Villa ilikubali kulipa sehemu kubwa ya mshahara wake ili kumpata.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 27, ambaye ni zao la akademi ya Man United, ameendelea kufanya mazoezi katika kituo cha Carrington pamoja na wachezaji wengine ambao hawapo katika mipango ya Amorim, akiwemo Antony na Alejandro Garnacho.
Rashford kwa muda mrefu ameonesha wazi ndoto yake ni kujiunga na Barcelona, ingawa klabu hiyo pia iliwahi kufikiria kumsajili Luis Diaz wa Liverpool.
Mwezi uliopita alipohojiwa kama angependa kucheza na staa wa Barca, Lamine Yamal, alisema:
“Ndiyo, bila shaka. Kila mtu anataka kucheza na wachezaji bora zaidi. Tumwombe Mungu- tutaona.”
Iwapo uhamisho huu wa mkopo utaenda kama ulivyopangwa na Rashford atasaini mkataba wa kudumu msimu ujao, itamaliza safari yake ya miaka 20 ndani ya Man United na katika kipindi chote amecheza mechi 426 na kufunga mabao 138, akiwa ameshinda Europa League, Kombe la FA mara mbili, na Kombe la Carabao mara mbili.
Kocha wa timu ya taifa ya England, Thomas Tuchel, alimjumuisha katika kikosi Machi, jambo lililoonesha matumaini anaweza kurudi kwenye kikosi cha Kombe la Dunia la msimu ujao.