Ishu ya Man United, Baleba aachiwa msala
Muktasari:
- Baleba, 21, amewekwa mstari wa mbele na Man United katika wachezaji inaowasaka katika dirisha hili, hasa katika eneo la kiungo mkabaji.
BRIGHTON, ENGLAND: KIUNGO Carlos Baleba ameachiwa msala wa kulazimisha uhamisho wake wa kwenda kujiunga na Manchester United baada ya miamba hiyo ya Old Trafford kupunguza kasi kidogo ya kunasa saini ya staa huyo katika dirisha hili.
Baleba, 21, amewekwa mstari wa mbele na Man United katika wachezaji inaowasaka katika dirisha hili, hasa katika eneo la kiungo mkabaji.
Mazungumzo yalianza na klabu ya Brighton mapema mwaka huu baada ya Man United kutuma watu wake. Baada ya hapo, klabu hizo zilifanya mazungumzo ya moja kwa moja, huku Brighton ikiweka wazi haitaki kumuuza Baleba.
Brighton imeiambia Man United itawagharimu hadi Pauni 120 milioni wakijaribu kuvuna pesa nyingi kuliko iliyovuna kwenye mauzo ya kiungo Moises Caicedo kwenda Chelsea mwaka 2023 ili wao wakubali kumruhusu Baleba aondoke.
Na ripoti zinafichua kwamba, Man United haipo tayari kulipa hiyo pesa kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi.
Kocha wa Brighton, Fabian Hurzeler alisema anaamini Baleba atabaki kwenye kikosi chake kwa sababu hayo ndiyo matumaini yake.
Man United imeshafanya usajili wa Pauni 207.5 milioni kwa kuwanasa Matheus Cunha, Bryan Mbeumo na Benjamin Sesko. Wachezaji wote hao ni washambuliaji na sasa kipaumbele cha kocha Ruben Amorim ni kusajili kiungo, hasa Namba 6.
Man United imechagua kuwa wapore na huenda wakarudi upya kwenye meza ya mazungumzo mwakani la itatafuta mbadala na kumsajili dirisha hili.
Kwa kiungo Baleba ishu ya makubaliano binafsi hilo haliwezi kuwa tatizo na sasa kinachokwamisha usajili wake ni Brighton kutaka pesa nyingi.
Hata hivyo, hakuna uthibitisho kama Baleba hafurahii huko Brighton. Huko Old Trafford mabosi wana imani kubwa Baleba anaweza kufanya jambo la kulazimisha mambo ili akavae uzi wa Man United msimu huu.