Iran yajadiliana na FIFA kuhamishia mechi nje Marekani
Muktasari:
- Ubalozi wa Iran nchini Mexico umesema mamlaka ya soka ya nchi hiyo inataka mechi zao zifanyike Mexico badala ya Marekani.
Iran imesema iko kwenye mazungumzo na FIFA kuhusu uwezekano wa kucheza mechi zake za Kombe la Dunia nje ya Marekani, baada ya Donald Trump kuionya timu hiyo kukaa mbali na nchi hiyo wiki iliyopita.
Ubalozi wa Iran nchini Mexico umesema mamlaka ya soka ya nchi hiyo inataka mechi zao zifanyike Mexico badala ya Marekani.
Hata hivyo, inaaminika kuwa FIFA haiko tayari kubadilisha ratiba ya mechi huku ikiwa imesalia chini ya siku 100 kabla ya mashindano kuanza.
“Wakati Trump amesema wazi kuwa hawezi kuhakikisha usalama wa timu ya taifa ya Iran, hatutasafiri kwenda Marekani,” alinukuliwa akisema Mehdi Taj, rais wa Shirikisho la Soka la Iran.
“Kwa sasa tunafanya mazungumzo na FIFA ili mechi za Iran katika Kombe la Dunia zifanyike Mexico.”
Kutokuwepo kwa uhakika kuhusu ushiriki wa Iran kumeongezeka tangu kuzuka kwa mgogoro kati ya Marekani na Israel. Alhamisi iliyopita, Trump alizungumzia suala hilo kupitia mtandao wake wa Truth Social.
“Timu ya taifa ya soka ya Iran inakaribishwa kwenye Kombe la Dunia, lakini sidhani ni sahihi wao kuwepo huko kwa sababu ya usalama wao wenyewe,” aliandika Trump.
Kauli zake zilikuja siku moja baada ya Taj kuashiria kuwa timu hiyo inaweza kususia mashindano hayo, kufuatia mashambulizi ya Marekani na Israel yaliyodaiwa kumuua kiongozi mkuu wa Iran na kusababisha mashambulizi ya kulipiza kisasi.
Waziri wa Michezo wa Iran, Ahmad Donyamal, alisema kuwa “hakuna mazingira yoyote” ambayo Iran inaweza kushiriki, na kwamba “hakuna uwezekano” wa timu hiyo kushiriki kwenye mashindano hayo.
“Tangu serikali hii ilipomuua kiongozi wetu, hatuna mazingira yoyote ya kushiriki Kombe la Dunia,” alisema Donyamal katika mahojiano ya televisheni.
“Kwa kuzingatia hatua mbaya zilizochukuliwa dhidi ya Iran, tulilazimishwa kuingia katika vita viwili ndani ya miezi nane au tisa, na maelfu ya watu wetu waliuawa. Hivyo hatuna kabisa uwezekano wa kushiriki kwa hali hii.”
Alipoulizwa kuhusu ushiriki wa Iran katika Kombe la Dunia wiki iliyopita na Politico, Trump alijibu: “Sijali kabisa.”
Iran imepangwa kucheza dhidi ya New Zealand, Ubelgiji na Misri katika mwezi ujao. Mechi zao mbili za kwanza zinatarajiwa kufanyika katika Uwanja wa SoFi jijini Los Angeles, huku mechi ya tatu ikipangwa kufanyika Seattle.
Ingawa Kombe la Dunia linaandaliwa kwa pamoja na Mexico, Canada na United States, idadi kubwa ya mechi itachezwa Marekani. Ikiwa Iran itafuzu kutoka kundi lake kwenda hatua ya mtoano, kuna uwezekano mkubwa italazimika kucheza Marekani.
Iwapo Iran itajiondoa rasmi, hiyo itakuwa mara ya kwanza katika enzi ya kisasa na itaiacha FIFA na jukumu la haraka la kutafuta timu mbadala.
Shirikisho la Soka la Asia, (AFC), lilisema Jumatatu kuwa halijapokea taarifa yoyote kwamba Iran itajiondoa kwenye mashindano hayo.
“Mwisho wa siku, ni shirikisho lenyewe ndilo linapaswa kuamua kama watacheza, na hadi leo wametuambia wanaenda Kombe la Dunia,” alinukuliwa akisema Windsor John kupitia Reuters.